Na:
Calvin Gwabara –Tanga.
Mkoa wa
Tanga umepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa programu za mafunzo ya jamii
(CBT) zinazolenga kuboresha mbinu za kilimo, kuwawezesha wakulima wa ndani, na
kuimarisha uwezo wa taasisi mbalimbali na kuchangia kuhimili mabadiliko ya
tabia nchi.
![]() |
Picha ya pamoja ya wakulima viongozi kutoka vijiji vya Mashindei, Vugiri, Old Ambangulu na Bagamoyo wakati wa mafunzo ya Kilimo Hifadhi na mbinu za kuhimili mabadiliko ya tabianchi Wilayani Korogwe. |
Akizungumza
kuhusu shughuli na mafanikio ya mradi, Bettie Luwuge, Meneja wa Mradi wa
FORLIVES, alisema kuwa mradi huu unahamasisha matumizi yenye usawa ya
rasilimali za asili kwa ajili ya maisha endelevu katika Milima ya Usambara
Magharibi, Tanzania na kutekelezwa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili
Tanzania (TFCG) kwa ufadhili wa Danmission. Mradi unashirikiana karibu sana na
Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.
Mradi umejikita
kwenye mafunzo na kuijengea uwezo jamii na makundi mbalimbali umefanya mafunzo kwa wakulima, viongozi wa
dini, na maafisa wa kilimo katika wilaya za Korogwe, na Lushoto na kutoa elimu
kwa vitendo, hali iliyochochea maendeleo
endelevu katika mkoa huo na uendelevu katia uwakili wa maliasili.
Meneja
huyo wa Mradi amesema moja ya mambo muhimu yaliyofanyika ni mafunzo kwa
wakulima viongozi (CBT) huko Korogwe katikati ya mwaka jana, yaliyolenga
kuwawezesha wakulima kwa mbinu za kisasa za kilimo, uhifadhi wa mazao baada ya
mavuno, na uunganishaji wa masoko ambapo washiriki walipata uelewa wa kina juu
ya jinsi ya kuongeza uzalishaji na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno,
jambo ambalo limekuwa changamoto kwa wakulima wadogo wa eneo hilo.
“Mradi
huu pia ulifanya ziara ya mafunzo kwa wakulima viongozi huko Muheza ambao
washiriki na kupata fursa ya kuona kilimo cha mazao ya viungo, uhifadhi wa
misitu, mnyororo wa thamani wa mazao ya viungo na miradi ya kilimo
iliyofanikiwa na kutumia mbinu bora katika maeneo yao, wakulima na maafisa
ugani walishirikiana na wataalamu wenye uzoefu na kujadili njia bunifu za
kuimarisha ustahimilivu wa kilimo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na wadudu,” alifafanua
Bi.Luwuge.
Aliongeza
“Mafunzo mengine muhimu yalifanyika Lushoto na yalihusu ujenzi wa uwezo wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (ELCT- NED) – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki
ambapo viongozi mahili akiwemo Baba Askofu Msafiri Mbilu (PhD), Sheikhe Kunguru na wengine kutoka Kamati ya Amani ya
Wilaya ya Lushoto ambapo mafunzo yalilenga kuimarisha viongozi wa dini na
watumishi wake katika Dayosisi kuhusu Uwakili wa maliasili, kuhimili na kustahimili
mabadiliko ya tabia nchi, Iko-Thiologia usimamizi wa migogoro, utawala bora ,
ushawishi, sera na sheria na namna ya kutumia membari kufikisha ujumbe wa
uhifadhi na uwakili wa maliasili kwa jamii”.
Kwa
mujibu wa Bettie Luwuge, changamoto kubwa iliyoonekana katika mafunzo yote ni hali ya matokeo ya athari za mabadiliko ya
tabianchi yalioathiri mwenendo wa mvua, uwezo mdogo wa kifedha kwani Wakulima
wengi wadogo wanakabiliwa na changamoto za gharama na ukosefu wa mikopo.na
miundombinu duni katika baadhi ya maeneo imeathiri utekelezaji mzuri wa
programu za mafunzo ya kilimo ingawa licha ya changamoto hizo, mafunzo hayo
yameleta mafanikio makubwa.
“Wakulima
wameripoti ongezeko la uelewa na maarifa kuhusu kilimo kinachozingatia
mabadiliko ya tabianchi, matumizi endelevu ya ardhi, na usimamizi bora wa
mifugo na tayari wengine wameanza kutumia mbinu mpya za kilimo kama vile kilimo
cha matuna, mafanya juu fanya chini, kilimo cha mtaro, kuchanganya mazao, kilimo
cha kontua, kilimo cha kufunikia mazao, kutotumia moto n.k ili kulinda ardhi,
kutunza maji na kupunguza mmomonyoko wa ardhi, jambo lililosababisha mavuno
bora na ongezeko la kipato,” alisema Luwuge.
Kwa mujibu
wa Bettie Luwuge, ziara ya kujifunza huko Muheza ilionyesha umuhimu wa ushirikiano
kati ya wadau mbalimbali kwa kuwaleta pamoja wakulima, watafiti, na maafisa wa
kilimo kwa kuunda jukwaa la kubadilishana maarifa kuongeza hamasa ya kilimo cha
mazao ya viungo na mnyororo wa thamani yake katika Wilaya ya Korogwe.
Akizungumzia
mafunzo hayo Sheikh Baruti kwa niaba ya viongozi wa dini wa wilaya ya Lushoto
amesisitiza hitaji la kuwa na programu za maendeleo zilizopangiliwa vizuri
ndani ya taasisi za kidini na umuhimu wa kutumia nafasi zao za uongozi wa dini kuhamasisha
miradi ya uwezeshaji wa jamii zaidi ya utoaji wa huduma za kiroho,” alisema
Luwuge.
“Binafsi, nahisi nimepewa jukumu kubwa,
maana nahusika kwenye Mpango wa Baraka na Amani katika Baraza la BAKWATA, jukumu
hili la kuhamasisha ujuzi tuliojifunza hapa kwa wenzangu ni muhimu ili uweze kuenea
kwa waumini wote hivyo nina furaha na nipo tayari kuanza upya.”Alisema
Sheikhe Baruti.
Kwa
upande wake Askofu Joseph Mbilu alisisitiza washiriki wa mafunzo yaliyofanyika
Lushoto kuwa hata kazi ianyofanywa na mradi huo ni kazi ya Mungu kwakuwa
inawajengea uwezo watu kuweza kufanya kazi na kuzalisha kwa tija ili kujiletea
maendeleo.
![]() |
Baba Askofu DKT. Msafiri Mbilu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (ELCT- NED) – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki akizungumza kwenye mafunzo hayo. |
“Jambo moja
kuu ambalo lipo wazi katika maandiko, kwamba tumekosa katika zamani na sasa ni
lazima tusimame na tuendelee mbele, Sauti ya Mungu kupitia Yeremia 2:7
inatufundisha: “Nalikuletea katika nchi ya rutuba ili ule matunda yake na
mazao yake yaliyojaa; lakini mlijia na kuichafua nchi yangu na kuihatarisha
urithi wangu.” Warsha hii inapaswa kutuongoza kurudi katika njia sahihi”alisisitiza
Askofu MBilu
Aliongeza
“Wataalamu wamependekeza uwekezaji mkubwa zaidi katika huduma za ugani na
programu za ujenzi wa uwezo ili kuendeleza athari chanya za mafunzo haya hivyo
kuna kuna haja ya sera zinazosaidia upatikanaji wa fedha na pembejeo za kilimo
kwa wakulima wa vijijini na kupanua mafunzo haya katika wilaya nyingine
kutasaidia kufanikisha maendeleo endelevu ya kilimo.”
Meneja
wa Mradi wa FORLIVES, Bettie Luwuge, amesema kuwa ili kuendelea mbele, wadau
wakiwemo serikali za mitaa, taasisi za kidini, na mashirika ya kilimo wanapaswa
kushirikiana ili kupanua miradi hii kwa msaada sahihi na mafunzo endelevu,
wakulima na viongozi wa jamii watakuwa na ujuzi wa kuleta mabadiliko chanya na
kuimarisha usalama wa chakula na kuwa na uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko
ya tabianchi katika mkoa huo.
Mafanikio
ya programu hizi ni ushahidi wa nguvu ya kushirikishana maarifa na maendeleo
yanayoendeshwa na jamii kwani kadri maeneo mengi yanavyoanza kutumia mbinu kama
hizi, Tanzania itanufaika kwa kuwa na sekta ya kilimo yenye ustahimilivu na
yenye tija zaidi.
Mradi
wa Uhifadhi wa Misitu, Haki na Maisha Bora kwa jamii (FORLIVES Project),
unahamasisha matumizi yenye usawa ya rasilimali za asili kwa ajili ya maisha
endelevu katika Milima ya Usambara Magharibi, Tanzania na unatekelezwa na Shirika
la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa ufadhili wa Danmission katika
Vijiji vinne ambavyo ni Mashindei (Kata ya Lewa), Vugiri, Old Ambangulu na
Bagamoyo (Kata ya Vugiri), Tarafa ya Bungu Wilaya ya Korogwe, Mkoa wa Tanga
![]() |
Kitalu cha miche ya mazao ya viungo aina ya Karafuu na Mdalasini kijiji cha Bagamoyo. Miche zaidi ya 6500 imeoteshwa kwa ajili ya wakulima kupanda mashambani mwao. |