Takribani kiasi cha tani millioni 7 za taka ngumu huzalishwa hapa nchini kwa mwaka ambapo wastani wa asilimia 45 hadi 50 tu hukusanywa na kutupwa dampo na vilevile asilimia 50 hadi 55 hubaki kwenye mazingira na kuzagaa kwenye mito na mifereji ya maji taka na mitaro ya maji ya mvua.
Hata hivyo, matokeo ya Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanaonesha kuwa, asilimia 40 ya kaya zinachoma taka ngumu na asilimia 22 ya kaya zinazotumia njia ya ukusanyaji wa mara kwa mara.
Ameyasema hayo leo Machi 30, 2025 jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuondoa Taka, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Amesema tafiti zinaonyesha pia zaidi ya asilimia 60 ya taka zinazozalishwa mijini zinaweza kuchakatwa au kutumika tena, lakini kutokana na changamoto za mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa taka, sehemu kubwa huishia kwenye madampo au kutupwa ovyo.
Aidha amesema serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na NEMC imeweka mikakati madhubuti ya kudhibiti taka kwa kutumia dhana ya Punguza, Tumia Tena na Rejeleza kama ilivyoainishwa katika Mwongozo wa Udhibiti wa Taka Ngumu.
“Serikali inahamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa za kuchakata taka, uwekezaji katika viwanda vya urejelezaji, na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa taka ili kuhakikisha taka zinapunguzwa, zinatumika tena, na zinachakatwa kwa ufanisi”. Amesema
Pamoja na hayo Naibu Waziri amezipongeza sekta binafsi kwa kuwekeza katika huduma ya uzoaji taka, urejelezaji na uchakataji wa taka ambavyo vinachangia katika kutoa ajira na kuimarisha usafi wa mazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesema dhana ya “Punguza, Tumia Tena na Rejeleza” ni msingi wa usimamizi endelevu wa taka na inahimiza matumizi bora ya rasilimali zetu ili kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Hata hivyo amesema uwekezaji katika teknolojia za uchakataji wa taka za nguo, kama mashine zinazoweza kuchakata pamba na polyester, utapunguza taka za nguo zinazotupwa na kuchafua mazingira.
Amesema wa kuzingatia dhana ya “Punguza, Tumia Tena na Rejeleza,” tunajenga jamii inayojali mazingira na kuchochea uchumi wa mzunguko ambao unalenga matumizi endelevu ya rasilimali.
“Katika sekta ya nguo na mitindo, tunahimiza matumizi ya malighafi rafiki kwa mazingira, mbinu bunifu za kubuni nguo zinazoweza kutumika kwa muda mrefu, na urejelezaji wa nguo na vitambaa ili kupunguza taka zinazoingia dampo”. Amesema Dkt. Semesi.
Amesema Baraza limejipanga kuhimiza na kuhakikisha kuwa dhana ya Punguza, Tumia Tena na Rejeleza katika sekta zote za uzalishaji inatekelezwa kwa vitendo ili kulinda mazingira yetu kwa kizazi cha sasa na kijacho.