NA WILLIUM PAUL, SAME.
WATU sita ambao ni Wanakwaya wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Chome wilayani Same mkoani Kilimanjaro, wamefariki dunia huku wengine 23 wakijeruhiwa baada gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Mwenyekiti wa ulinzi na usalama wilaya ya Same ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo, Kasilda Mgeni alisema kuwa ajali hiyo ilitokea leo majira ya asubuhi.
Alisema kuwa, wanakwaya hao walikuwa wakitokea Chome kuelekea Vudee kueneza Injili kwa njia za nyimbo ambapo walipofika barabara ya Bangalala wakapata ajali.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, chanzo cha ajali hiyo ni gari aina ya kosta walilokuwa wakisafiria lilipofika kwenye mlima lilishindwa kupanda na kuanza kurudi na kuangukia bondeni.
Alisema kuwa, majeruhi wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Same wakiendelea kupatiwa matibabu huku miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali hiyo.
Akithibitisha kupokea majeruhi hao, Mganga Mkuu wa wilaya ya Same, Dkt. Alex Alexander alisema kuwa, wamepokea majeruhi 23 ambapo wengi wao wamevunjika maeneo mbalimbali huku wemgine wakiwa na majeraha na wanaendelea kupatiwa matibabu huku hali zao zikiwa nzuri.
Dkt. Alexander alisema kuwa pia wamepokea miili ya watu sita waliofariki katika ajali hiyo ambapo imehifadhiwa katika chuma cha kuhifadhia marehemu kusubiria utambuzi wa ndugu zao.