Kampuni Tanzu ya TANESCO inayojishughulisha na Ujenzi pamoja na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) imetoa msaada wa vitu mbalimbali katika Kituo cha Kulea Watoto Igamilo kilichopo Mkoani Tabora ikiwa ni sehemu ya kuonesha mshikamano katika jamii pamoja kuwatakia kheri ya Sikukuu ya Eid el Fitri.
Msaada huo uliotolewa na ETDCO ni Mbuzi, Sukari, Sabuni, Mchele, Unga wa Ngano na Unga wa Sembe, Mafuta ya kupikia, Vifaa vya usafi, Soda, Biskuti.
Akizungumza wakati kukabidhi msaada huo, Machi 30, 2025 Mkoani Tabora kwa niaba ya Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Urambo, Mhandisi Ntuli Burton, amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya juhudi za Kampuni katika kusaidia jamii inayozunguka hasa maeneo wanayotekeleza Miradi.
Mhandisi Burton amesema kuwa msaada huo utawawezesha watoto kufurahi na kusherehekea sikukuu ya Eid el Fitri wakiwa na furaha kama watoto wengine wanaoishi na wazazi wao.
“Sisi kama Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya umeme tumeona ni jukumu letu kuhakikisha tunasaidia jamii inayotuzunguka, hususani maeneo ambayo tunatekeleza miradi, kama hapa Igamilo, Tabora ambapo tumetekeleza mradi wa kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Urambo,” amesema Mhandisi Burton.
Mkuu wa Kituo cha Kulea watoto cha Igamilo, Abu Salim ameishukuru Kampuni ya ETDCO kwa kutoa msaada huo ambao utawawezesha watoto kufurahia sikukuu ya Eid el Fitri.
“Natoa wito kwa jamii kuwakumbuka watoto walioko kwenye vituo vya Kulea watoto Yatima kama Kampuni Tanzu ya TANESCO, ETDCO ilivyofanya, kwa kufika na kutoa msaada” amesema Salim. Kituo hicho cha Kulea watoto cha Igamilo, Tabora kina jumla ya watoto 78.