Na Mwandishi wetu, Mirerani
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Olonyokie Ole Sendeka ameimba taarabu kwenye harusi ya Rogers Elisha na Angel, mtoto wa Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi.
Ndoa takatifu imefungwa na Askofu Sommy Severua wa madhehebu ya Desciple Nations Pentecost Church (DNPC) Mji mdogo wa Mirerani na sherehe za harusi katika ukumbi wa Dream Park mji mdogo wa Boma ng’ombe Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.
Ole Sendeka huku akishangiliwa na umati wa watu kwenye ukumbi huo wa Dream Park mji mdogo wa Boma ng’ombe, aliimba wimbo wa taarabu kupendwa bahati yangu simzizi kutumia amependa umbo langu.
“Kupendwaaa baaahati yaaangu simzizi kutumia aa amependa umbo langu nimewazidi mizunguuu,” ameimba mbunge huyo Ole Sendeka huku akishangiliwa na wa watu.
Akizungumza kwenye harusi hiyo Ole Sendeka amewaasa Rogers na Angel waishi kwa upendo na amani katika maisha yao ya kila siku katika ndoa.
“Rogers sasa umeoa utulie nyumbani na Angel pia umeolewa utulie na mwenzako kwani yeye ndiye mwanaume pekee aliyekuoa,” amesema Ole Sendeka.
Ole Sendeka aliwazadia maharusi hao dola 300 kwa ajili ya kutumia pindi wakiwa kwenye fungate yao mara baada ya harusi yao.
“Pamoja na kutoa ng’ombe mmoja kwenye maandalizi ya harusi yenu nawaongezea pia ng’ombe wawili kama zawadi ya harusi yenu,” amesema Ole Sendeka.
Mbunge huyo ambaye aliongozana na viongozi mbalimbali pia walijitolea zawadi ya ng’ombe, mbuzi na kondoo katika harusi hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga alijitolea zawadi ya ng’ombe mwekundu na Diwani wa Kata ya Shambarai Julius Lendauwo Mamasita naye alijitolea zawadi ya ng’ombe mmoja.
Mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa vijana UVCCM Wilaya ya Simanjiro, Timothy Ngoyai Lengitambi alijitolea zawadi ya mbuzi na Diwani wa viti maalum alijitolea zawadi ya kondoo kwa maharusi hao.

