Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke,akizungumza na waaumini wa Kiislamu baada ya Sala ya Idd El Fitri,leo katika Uwanja wa Nyamagana.
………….
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
SHEIKH wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke,amewaonya vijana kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 kuwa wasikubali kushawishiwa na baadhi ya wanasiasa kutumika vibaya kwa kuvuruga amani ya nchi.
Akizungumza katika sala ya Idd el Fitri iliyofanyika leo, kimkoa katika Uwanja wa Nyamagana,Sheikh Kabeke amesisitiza umuhimu wa amani na utulivu kipindi hiki cha uchaguzi, akiwataka Waislamu kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi kupitia vyama vya siasa kwa kuwa wanayo sifa ya kuwa raia wa nchi hii.
“Amani ni kila kitu, furaha tunayopata hapa nchini ni kutokana na amani tuliyonayo, na ndio maana leo hii tumekusanyika hapa kwa ajili ya kusali Sala ya Idd,” amesema na kuongeza kuwa amani ndiyo kiungo muhimu kinachowafanya Watanzania kuishi kwa utulivu ambapo aliwahimiza Waislamu kuheshimu amani kwani dini ya Kiislamu inahamasisha amani na unyenyekevu.
Akizungumzia uchaguzi,Sheikh Kabeke amesema mwaka huu ni kipindi cha uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge, na Madiwani, lakini baadhi ya vyama vya siasa ( bila kutaja majina),tayari vinaonyesha viashiria vya kuvunja amani huku akiwatahadharisha viongozi wa dini na Watanzania wenye mapenzi mema kuwa wanapaswa kukemea vyama vya siasa vinavyoshirikisha viashiria vya vurugu.
“Nitoe wito,ni muhimu kwa viongozi wa dini na Watanzania kuungana na kusema ‘hapana’ kwa chama chochote cha siasa kinachovunja amani”alisema kuongeza kuwa Watanzania zaidi ya milioni 60 wengi wao licha ya kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa,bado wana haki ya kushiriki uchaguzi na kuamua mustakabali wa nchi yao,”amesema.
Sheikh Kabeke amewataka vijana wa Kiislamu na wa Kitanzania kwa ujumla kutunza amani na kuepuka kuwa chombo cha vurugu na kutahadharisha, ikiwa wanasiasa wanataka kuamua mustakabali wa nchi yetu pekee yao kwa kuhamasisha vurugu,hilo halitakubalika.
Amewakumbusha viongozi wa kisiasa wanaohubiri kuwa “tutaleta fujo” au “tutavunja amani,” wanawaandaa watu kwa madhara yanayoweza kuathiri jamii nzima,hivyo amani ikivurugika, hakuna mahali pa kwenda zaidi ya hapa Tanzania pekee,hivyo tunawajibika kuilinda nchi yetu na vijana wa kiislamu na kitanzania,katu msikubali miili yao kutayarishwa kwa ajili ya kufanya fujo.
“Tumeanza kusikia maneno kwamba tutaleta fujo, uharibifu na kuipasuapasua nchi kwa nguvu ya umma,mtu anayesema hayo tafsiri na maana yake anawaandaa watu waingie barabarani wakafanye maandamano ,”amesema Sheikhe Kabeke.
Amesema katika hilo hakuna kulemba ni vyema wanasiasa wenye nia hiyo waambiwe ukweli kuwa,nchi zingine amani ilipovurugika mustakabali wao ni hapa nchini,hivyo tunawajibika kuilinda nchi yetu na amani iliyopo.
Aidha, ameeleza kuwa vijana wanapoambiwa na viongozi wao wa kisiasa wanapaswa kutafakari kwa makini kabla ya kujiunga na maandamano au shughuli yoyote inayoweza kusababisha machafuko, madhara yake yataathihiri familia zao na jamii kwa ujumla.
Kiongozi huyo wa kiroho amesema kuwa Serikali ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imeanzisha mfumo wa 4R,unaotoa fursa ya kuzungumza na kuridhiana, hivyo ni vyema kutumia fursa hiyo ili kuleta mabadiliko ya amani.
Sheikh Kabeke amewahimiza Waislamu na hata wasio Waislamu kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi kupitia vyama vya siasa wanavyoona vinafaa kwa sababu si vyote ving’aavyo ni dhahabu na akili za kuambiwa wachanganyanye na za kwao.
Amesema,“Si vyema kusema uchaguzi siyo wetu, kila Mwislamu ni raia wa nchi hii na anayo haki ya kugombea, kuchagua, na kuchaguliwa kama ilivyo kwa raia wengine.”
Sheikh Kabeke na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Mwanza,amesisitiza umuhimu wa amani, ushiriki wa wananchi katika uchaguzi na kuepuka ushawishi wa kisiasa unaoweza kuhatarisha umoja na utulivu wa nchi.
“Mtume S.A.W anasema kufikiri saa moja ni bora kuliko ibada ya mwaka mzima pia, unapotaka kufanya jambo litazame hadi mwisho ,likiwa la heri fanya na likiwa la shari acha.Amani ni kama yao,ni lulu, ni kama yai likivunjika huwezi kuliungaunga, tutunze amani ya nchi tusikubali ushawishi wa aina yoyote,”amesema.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Baraza la Wazazi Mkoa wa Singida, Ahmed Misanga,amesema mwaka huu wa uchaguzi hategemei vijana kujitoa ufahamu kwa kurubuniwa na wanasiasa wenye malengo ya kuvuruga amani ya nchi.
“Vijana wanategemewa na taifa kujenga uchumi wake,serikali sasa imeboresha maisha yao na wengi wanafanya kazi,wapo wanaonufaika kwa mikopo asilimia kumi isiyo na riba kutoka halmashauri ili kujiinua kiuchumi,hivyo wasidanganywe na wana siasa kwenda kuvuruga amani,”amesema.
Misanga amesema mwanasiasa anayewadanganya na kuwahamasisha kuingia mitaani kufanya vurugu,hawawezi kuinuka na familia yake zaidi ya kujificha,ikitokea amepata madhara katika vurugu atatibiwa nje ya nchi .
“Wewe kijana unayehaingaka na kesho yako kwa maisha ya kuunga unga kupitia ujasiriamali utatibiwa kwa gharama kubwa tena kwa kujificha,utakuwa unatafutwa na dola mithili ya mhalifu kwa kufanya vurugu,”amesema.
Misanga amesema wanasiasa wanaohubiri bila mabadiliko hakuna uchaguzi, Tanzania ni kubwa kuliko chama chochote na watanzania hawaamini katika vurugu,hivyo hawawezi kusikiliza maneno ya chama kimoja kati ya takribani vyama 20 vya siasa.