
Waendesha pikipiki maarufu kama boda boda, wajasiriamali, na baadhi ya wananchi wa Kata ya Ngemo, wilayani Mbogwe, mkoani Geita, wameonyesha kuguswa na utendaji kazi wa Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Nicodemas Maganga, kwa kuchangia fedha zitakazomsaidia kununua fomu ya kuwania tena nafasi hiyo katika uchaguzi ujao.
Tukio hilo lilifanyika wakati wa mkutano wa hadhara ulioandaliwa katika kata hiyo, ambapo viongozi wa chama, serikali, na wananchi wa vijiji mbalimbali walihudhuria.
Wananchi hao wamesema wameendelea kutambua jitihada kubwa zinazofanywa na mbunge wao, hususan katika kuwawakilisha na kuwatetea ili kuhakikisha maendeleo yanafika katika maeneo yao. Kwa kutambua mchango wake, wameamua kumuunga mkono ili apate fursa ya kuendelea kuwatumikia kwa awamu nyingine.