Katika kukabiliana na changamoto ya vitendo vya kikatili ambavyo vimekuwa vikilikumba kundi la vijana ikiwemo mila zilizopitwa na wakati hususani ukeketaji na tohara isiyo salama Shirika la Grumet Fund limeanza kutoa elimu kwa vijana wa kike na kiume ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Sambamba na hilo Shirika hilo pia linatoa elimu juu ya kukabiliana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ambayo imekuwa ikipelekea mmomonyoko wa maadili kwa vijana.
Akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Serengeti iliyoko wilayani Serengeti mkoani Mara, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Grumet Fund Frida Mollel amesema Shirika hilo limefikia hatua hiyo baada ya kuona wasichana wakipitia changamoto kukeketwa, ndoa za utotoni na haki ya kutopata elimu.
Mollel amesema walianza kutoa elimu hiyo ili kunusuru kundi hilo ambalo linazidi kuathirika kwa kiwango kikubwa.
Zaidi ya vijana elfu tano (5000) wamefikiwa na elimu hiyo kwa mwaka 2024 huku shirika hilo likiendelea kutoa elimu kwa vijana hususani wa vijijj na Shule zinazozunguka mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumet.