Kutoka Kulia Katibu wa Chama cha Umoja wa Makandarasi na watoa Huduma shirikishi (TUCASA) Daniel Materu na Meneja Mkazi wa PUM, Tanzania, Peter Van Den Hoek wakisaini mikataba ya makubaliano kwaajili ya Kuboresha Sekta ya Ujenzi Nchini Tanzania.

Mwenyekiti wa Chama cha Umoja wa Makandarasi na watoa Huduma shirikishi (TUCASA), Qs Samwel Marwa kushoto akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini mikataba ya makubaliano kwaajili ya Kuboresha Sekta ya Ujenzi Nchini Tanzania. Kulia ni Katibu wa Chama cha Umoja wa Makandarasi na watoa Huduma shirikishi (TUCASA) Daniel Materu.
Mwakilishi wa PUM nchini Tanzania, Deogratias Mbena akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini mikataba ya makubaliano kwaajili ya Kuboresha Sekta ya Ujenzi Nchini Tanzania.
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
CHAMA Cha Umoja wa Makandarasi na watoa Huduma Shirikishi Tanzania (TUCASA) kimesaini makubaliano na Chama cha Waholanzi Wastaafu wa Ujenzi, Netherlands Senior Expert (PUM), kwa lengo la kutoa ujuzi na maarifa katika sekta ya ujenzi hapa nchini.
Mkataba huu wa miaka mitano utalenga kuboresha ufanisi wa miradi ya ujenzi, kupunguza gharama za utekelezaji wa miradi, na kuongeza ubora wa kazi za ujenzi na miundombinu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Aprili 02, 2025, Mwenyekiti wa TUCASA, Qs Samwel Marwa amesema kuwa makubaliano hayo yatatoa fursa kwa wakandarasi na wataalamu wa ujenzi nchini Tanzania kupata mafunzo ya kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa ujenzi wa Uholanzi, ambao watashirikiana na wahusika katika sekta ya ujenzi hapa Tanzania.
“Hii itasaidia kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi, kuboresha mbinu za kisasa za ujenzi na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora wa hali ya juu na kwa gharama nafuu.”
Ameelezea furaha yake kwa kushirikiana na PUM, na kusema kuwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba sekta ya ujenzi nchini Tanzania inaendelea kukua na kutoa matokeo bora zaidi.
Amesema …”Makubaliano haya yatasaidia kuboresha usimamizi wa miradi yetu ya ujenzi, kupunguza changamoto za gharama na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu, jambo linalozingatia malengo ya taifa ya maendeleo endelevu.”
Kwa upande wao, Mwakilishi wa PUM, Deogratias Mbena aneeleza furaha yao kwa kushirikiana na TUCASA katika juhudi za kukuza sekta ya ujenzi nchini Tanzania.
Pia amesisitiza kwamba mafunzo ya kitaalamu na ushirikiano wa karibu kati ya wataalamu wa Uholanzi na Tanzania utasaidia kuboresha ufahamu wa wakandarasi na wataalamu wa ujenzi hapa nchini.
“Wataalamu wa Kiholanzi watatoa mafunzo na ushauri kuhusu mbinu bora zausimamizi wa miradi, kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.”
pia amesema ushirikiano huo utasaidia kubaini na kuondoa mianya ya upotevu wa rasilimali, hivyo kupunguza gharama za utekelezaji wa miradi, pamoja na
Wataalamu wa Kiholanzi watashirikiana na wakandarasi wa Tanzania kubadilishana ujuzi na teknolojia za kisasa katika sekta ya ujenzi.
Makubaliano haya ni hatua muhimu katika kuboresha sekta ya ujenzi na miundombinu nchini Tanzania, na yanatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wakandarasi na kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania (Ambassador for the Embassy of the Kingdom of Netherlands), Wiebe de Boer kushoto akizungumza walipokutana na Wanachama wa Chama Cha Umoja wa Makandarasi na watoa Huduma Shirikishi Tanzania (TUCASA) jijini Dar es Salaam leo Aprili, 02, 2025.

Picha ya Pamoja.