Mbunge wa Jimbo la Manonga wilayani Igunga mkoani Tabora Seif Khamis Gulamali wa tatu kutoka kushoto akiwa na baadhi ya viongozi, kushoto mwenyekiti wa CCM wilaya ya Igunga Mafunda Temanya.
Na Lucas Raphael,Tabora
MBUNGE wa Jimbo la Manonga Seif Khamis Gulamali amesema kuwa Serikali imekwisha toa kiasi cha shilingi bilioni 3 ili kukamilisha shule ya amali ambayo inajengwa katika kata ya Choma Wilayani Igunga mkoani Tabora.
ALItoa taarifa hiyo April 1, 2025 wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Choma kwenye hafla ya dua ya kuwaombea ndugu na jamaa waliotangulia mbele za haki.
Alisema kuwa tayari Serikali imetoa kiasi cha shilingi 602,000,000 awamu ya kwanza na ujenzi umeanza chini ya Mkandarasi Bajeso Investment Group of Companies LTD kutoka jijini Mwanza.
Aidha alisema shule hiyo itakapokamilika itachukua wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita na kuongeza kuwa shule hiyo itakuwa ya bweni ambapo tayari ujenzi ulishaanza tangu mwezi 3/2025 na utachukua muda wa miezi sita mpaka kukamilika kwake.
Aidha mbunge huyo alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuendelea kuitunza miradi yote inayoletwa na serikali katika maeneo yao.
“Ndugu zangu wananchi mimi kama mbunge wenu nawaombeni sana muitunze miradi yote inayoletwa na serikali kwani mtakapoitunza itawasaidia hadi vizazi vijavyo kwa kuwa serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kutekeleza miradi hiyo.” Alisema Gulamali.
Sambamba na hayo mbunge huyo alisikitishwa na kitendo cha baadhi ya wagombea ubunge ambao wamekuwa wakipita kwenye jimbo hilo la Manonga na kujinadi huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume na utaratibu wa Chama Cha Mapinduzi.
Ambapo aliwaomba wanaofanya hivyo waache na kusubiri hadi muda utakapofika kwani kwa sasa yeye ndiye bado mbunge wa jimbo la Manonga.
Kwa upande wake Fredrick Mwita Mhandisi anayetekeleza mradi huo, alisema kuwa tayari wamekwisha anza ujenzi wa madarasa nane (8), jengo la TEHAMA, Maktaba, Maabaara, Jengo la Utawala, vyoo na nyumba ya mtumishi.
” Tumepokea kiasi cha shilingi 602,000,000 kwa ajili ya ujenzi huo kwa awamu ya kwanza na tunatarajia kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi kwa miezi sita,” alisema Mhandisi Frederick Mwita.
Nao baadhi ya wananchi, Albert Nicodemus Panga, Mwamvua Rajabu na Rehema Juma kwa nyakati tofauti walisema “ Mradi huo umekuja kutatua tatizo la wanafunzi kutembea umbali mrefu kutafuta elimu, kwa hiyo wanafunzi wanaotoka Bulangamilwa, Bulyambelele na maeneo jirani watapata elimu katika shule hiyo.
Ambapo Rais Dkt Samia Suluhu Hassani kupitia mradi huo amewapunguzia adha wanafunzi hao ili kila mmoja apate elimu kwa karibu, na pia inabadilisha maisha ya jamii hizo na kukuza uchumi.
Ambapo huo mradi unakuja kubadilisha taswira na kuleta fursa za ajira kwa wananchi wa kata ya choma, kwa kuwa watu watafanya biashara kupitia mradi huo na watumishi watakaokuja katika eneo hilo nao watanufaika.
Naye Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi CCM wilaya ya Igunga Peter Oronge alitumia fursa hiyo kwa kuwambusha wanachama wote wa CCM waliojiandikisha kidigitali kwenda kwenye matawi ya kata zao kuchukua kadi zao za kielektroniki, na kwa wale ambao bado pia wafike katika ofisi hizo za CCM kujiandikisha bure ili wawe na kadi hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Igunga Mafunda Temanya aliwataka Wana CCM Igunga kuwa wamoja na kuacha kutumia mitandao ya kijamii kutoa lugha za matusi na kuleta taharuki ikiwa pamoja na kuchonganisha viongozi na wanachama wenyewe.
Pia alitoa onyo kwa wanachama ambao wanapita kwa wananchi na kuanza kupiga kampeni kabla ya muda kufika.
” Ndugu zangu naomba mnielewe, natoa onyo kwa wananchama wote ambao wanapita kwa wananchi na kuanza kujinadi au kunadi wanachama wengine muda wa kuanza kampeni bado, ndugu tukikubaini kufanya hivyo kinyume na utaratibu wa Chama tutakuita na kukuondoa katika kugombea ili sasa ukakae na hizo fedha zako huko nyumbani kwako, kuweni na subira muda ukifika tutatangaza kuanza kuchukua fomu za kugombea,” alisema Mafunda Temanya.