WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Aprili 2,2025 Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2024 kubadili machaguo ya tahasusi (Combination) na kozi mbalimbali wanazohitaji kusoma kulingana na ufaulu wao.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa,akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 2,2025 Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2024 kubadili machaguo ya tahasusi (Combination) na kozi mbalimbali wanazohitaji kusoma kulingana na ufaulu wao.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema wanafunzi waliomaliza Kidato cha Nne mwaka 2024 wanayo nafasi ya kubadili machaguo ya tahasusi (Combination) na kozi mbalimbali wanazohitaji kusoma kulingana na ufaulu wao.
Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Aprili 2,2025 Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa waandoishi wa habari kuhusu wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2024 kubadili machaguo ya tahasusi (Combination) na kozi mbalimbali wanazohitaji kusoma kulingana na ufaulu wao.
Mchengerwa, amesema kuwa rasmi sasa wahitimu wa Kidato cha Nne wa mwaka 2024 wanaweza kubadilisha machaguo ya tahasusi (combination) za kidato cha tano, vyuo vya kati, na elimu ya ufundi kupitia mfumo wa kielektroniki wa uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha tano na vyuo hivyo.
“Zoezi la kubadilisha tahasusi na vyuo lilianza rasmi Machi 31, 2025, na litakamilika Aprili 30, 2025. Hivyo, wanafunzi, wazazi, na walezi wanakumbushwa kushauriana kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu na kitaaluma, kabla ya kufanya mabadiliko ya tahasusi au kozi.”amesema Mhe.Mchengerwa
“Huduma hiyo ya kubadilisha tahasusi ni bure, na iwapo wanafunzi watakumbana na changamoto, wanapaswa kuwasiliana na Dawati la Huduma kwa Mteja kupitia barua pepe: huduma@tamisemi.go.tz au kupiga simu kwa namba +255 262 160 210 na +255 735 160 210.”amesisitiza Mhe.Mchengerwa
Itakumbukwa kuwa serikali imekuwa ikitoa fursa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne kufanya mabadiliko ya machaguo ya tahasusi (combination) na kozi mbalimbali walizozichagua kupitia Fomu ya Uchaguzi (Selform). Fursa hii huwawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya mtihani wa Kidato cha Nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).