Serikali kuwa itahakikisha wananchi, wakiwemo Waislamu ambao bado hawajaboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, wanapata fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kutokana na maboresho ya daftari yanayoendelea ili kila raia mwenye haki ya kupiga kura anafikiwa kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Mwafnza, Said Mtanda, amesema alipozungumza na waumini wa dini ya Kiislamu katika Baraza la Idd lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu (BOT),leo.
Mtanda amesema serikali inaendelea na maandalizi ya uchaguzi mkuu kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Tanzania, ikiwemo kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili kuhakikisha kila raia anapata haki ya kupiga kura.
“Kwa wale ambao bado hawajaboresha taarifa zao, nawataka waondoe hofu, kwa sababu serikali inaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha kila mmoja anafikiwa kwa wakati. Hii ni fursa kwa wananchi wote, na kila mmoja atapata nafasi ya kushiriki kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu,” amesema.
Mtanda amewashukuru wananchi wa Mwanza, waislamu na wasiokuwa waislamu, kwa juhudi zao za kudumisha amani na utulivu mkoani humu, akisema kuwa amani ni muhimu kwa ustawi wa taifa letu, kwamba amani haichagui dini, kabila, rangi, wala hali ya kiuchumi, amani ni kama yai; likivunjika, halirekebishwi tena.
Aidha, amewakumbusha wazazi na walezi wajibu wao katika malezi bora ya watoto kuwa, malezi bora ni haki ya kila mtoto, wazazi wanapaswa kutoa malezi yanayozingatia imani ya dini na maadili ya taifa na hivyo amewahimiza wazazi kuwalea watoto wao kwa upendo na kuzingatia haki zao, akiwataka pia kuwalinda dhidi ya ukatili wa aina yoyote.
“Malezi bora ya watoto ni haki yao, na hii inaanzia nyumbani. Wazazi wanawajibika kuwalea watoto kwa kutoa malezi ya kimwili, kiroho na kuhakikisha wanapata lishe bora. Hii ni muhimu ili tuweze kujenga taifa lenye maadili bora,” amesisitiza Mtanda.
Mkuu huyo wa mkoa amesema, mbali na malezi ya kijamii na kiroho, wazazi wanapaswa kuandika wosia na mirathi, ili kupunguza migogoro katika familia baada ya kifo,kufanya hivyo ni kuimarisha amani na utulivu katika familia na jamii kwa ujumla.
Pia, amewahimiza vijana wa Kiislamu na wasiokuwa Waislamu kutafuta elimu kwa bidii. akisema serikali inaendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga shule mpya na kuboresha miundombinu ya elimu.
Amefafanua kuwa katika mwaka 2024 pekee, serikali imetumia sh. bilioni 60 kuboresha miundombinu ya elimu,walimu 1,161 wameajiriwa mkoani Mwanza, amewahimiza vijana kuchangamkia fursa hiyo na kujitahidi kupata elimu bora.
“Kila mmoja wetu anapaswa kutafuta elimu kwa bidii. Serikali inaendelea kufanya juhudi katika kuboresha sekta ya elimu, na kwa sasa tunajivunia kuanzisha shule mpya 85 za msingi na 30 za sekondari. Hii ni fursa kubwa kwa vijana wetu, na tunataka kuona kila mmoja akichangamkia fursa hii,” ameeleza Mtanda.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, pia amesisitiza umuhimu wa amani katika taifa letu, akisema kuwa Baraza la Idd ni fursa nzuri kwa serikali kuzungumza na Waislamu baada ya mwezi wa Ramadhani ambapo BAKWATA imejizatiti kujenga vituo vya afya saba mkoani humu, hivyo kusaidia juhudi za serikali katika kuboresha huduma za afya.
Katibu Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini, Askofu Robert Bundala, amesisitiza umuhimu wa umoja na amani, akisema Wakristo na Waislamu wanapaswa kushikamana na kuendelea kulinda amani ya nchi yetu, ni mali adhimu, ambayo ni rahisi kupoteza lakini ni ngumu kuipata tena.
“Katika uchaguzi huu, tusijiingize katika matabaka ya kidini au kikabila. Kila mtu anapaswa kuchagua kiongozi bora kwa maslahi ya taifa letu, na tuendelee kuishi kama wamoja,” amesema Bundala.
Sheikh Baruti wa Istiqama amesisitiza kuwa vijana ni nguzo muhimu ya taifa na wanapaswa kutambua wajibu wao katika kulinda amani huku akiwahimiza kuchukua nafasi yao katika kulinda amani wakati wa uchaguzi mkuu na kuepuka kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani.
Kwa upande wake, Abuu Maftaha wa Buhongwa Islamic ametoa wito wa kuendelea kujenga vituo vya afya na kutoa huduma bora kwa wananchi, kwamba kujenga vituo hivyo, wananchi wataweza kupata huduma bora za afya, huku akimpongeza Sheikh Kabeke kwa juhudi za kuendeleza miradi hiyo ya afya.
Kauli hizi zinaonesha dhamira ya pamoja ya viongozi wa dini na serikali katika kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 unafanyika kwa amani na utulivu, huku wananchi wote wakihamasishwa kuchangia maendeleo ya nchi yao kupitia elimu na ushiriki katika mchakato wa uchaguzi.