Na. John Masanja, IPALA
Awamu ya kwanza ya umeme wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umechochea shughuli za maendeleo na kuinua uchumi wa wananchi katika Kata ya Ipala, Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Kata ya Ipala, George Magawa wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofanya ‘media tour’ kutembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali katika kata hiyo kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya sita imepeleka huduma ya umeme katika Kata ya Ipala. “Kata yetu imefikiwa na awamu ya kwanza ambayo ina faida nyingi sana. Wananchi wanafanya shughuli mbalimbali zinazojumuisha matumizi ya umeme kwa kiwango kikubwa na naamini kwa siku za usoni hapa kwetu kutakuwa mtaa wa viwanda vya aina tofauti” alisema Magawa.
Nae mkazi wa Kata ya Ipala, Mathias Masita aliishukuru serikali kwa kuwapelekea umeme kwasababu maisha yao yamebadilika na wanafanya shughuli zinazohusisha umeme kwa kiwango kikubwa. “Mradi wa REA umetunufaisha sana, nakumbuka tulianza kutumia zile tochi za kawaida, tukaja kwenye umeme wa jua na sasa tumeletewa umeme halisi. Tumeingia kwenye mfumo ambao sasa hivi tuna viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza mafuta na mashine za kusaga nafaka. Tunaishukuru serikali kwa kutuletea umeme kwasababu manufaa ni makubwa sana” alishukuru Masita.
Kata ya Ipala ipo umbali wa kilomita 41 kutoka Dodoma mjini, Barabara kuu iendayo Hombolo. Wakazi wa kata hiyo ni maarufu kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji, ufugaji na umiliki wa viwanda vidogo vidogo vya kukamua alizeti na kukoboa nafaka.