Katika hatua ya kimkakati kusaidia wafanyakazi wa serikali kufikia malengo yao ya kifedha, benki ya Exim Tanzania inajivunia kutangaza maboresho katika huduma yake ya “Wafanyakazi Loan,” ambayo sasa inajumuisha suluhisho la uchukuaji wa mikopo.
Benki ya Exim imekuwa taasisi ya kwanza ya kifedha nchini Tanzania kuwezesha uchukuaji wa mikopo kwa wafanyakazi wa sekta ya umma kutoka taasisi zingine kupitia mfumo wa Utumishi Portal (ESS). Huduma hii ya kipekee inalenga kuwapatia watumishi wa umma masharti bora ya mikopo, uharaka wa upatikanaji wa fedha, na urahisi wa huduma kupitia jukwaa hili bunifu.
Mkuu wa Idara ya Wateja Wadogo na Kati kutoka Benki ya Exim Tanzania, Bw. Andrew Lyimo, alisisitiza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha wafanyakazi wa serikali wanapata suluhisho bora za kifedha. “Lengo letu ni kuwapatia wafanyakazi wa serikali huduma za kifedha zinazobadilisha maisha yao kimaendeleo. Kwa kuwachukulia mikopo yao kutoka taasisi nyingine, tunalenga kupunguza mzigo wao wa kifedha na kuwapatia masharti nafuu zaidi ya marejesho yanayolingana na mahitaji yao ya kifedha,” alisema Bw. Lyimo.
Wafanyakazi wa serikali sasa wanaweza kupata mikopo ya hadi TZS milioni 200, yenye muda wa kurejesha hadi miaka 10 (miezi 120). Kupitia ‘Wafanyakazi Loan’, Benki ya Exim inawawezesha watumishi wa umma kupata mtaji wa kifedha unaowawezesha kuanzisha au kupanua biashara zao, hivyo kujiongezea vyanzo vya mapato zaidi ya mishahara yao.
Bw. Lyimo aliongeza: “Tunatambua changamoto za kifedha zinazowakabili waajiriwa wa serikali, na kupitia mpango huu, tunalenga kuwasaidia kupata utulivu wa kifedha.”
Mbali na huduma ya uchukuaji mikopo, Mtenya Cheya, Mkuu wa Bidhaa na Uhakika wa Mapato, alieleza kuwa waombaji wa mikopo wataweza kuongeza kiwango cha mkopo wao kila baada ya miezi mitatu. Marejesho ya mkopo yatakuwa katika mfumo wa Malipo Sawa ya Kila Mwezi (EMI) kwa muda wote wa mkopo, hivyo kuwawezesha wateja kupanga bajeti zao kwa urahisi.
Aidha, mkopo huu unajumuisha bima ya maisha katika kipindi cha mkopo, ambayo inahakikisha kuwa deni linalobaki litalipwa endapo mkopaji atafariki dunia au kupata ulemavu wa kudumu. Hili linatoa amani ya akili kwa mfanyakazi na familia yake.