NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA
MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Dk. Dotto Bulendu, amezungumzia changamoto kubwa inayoikabili jamii ya kulishwa habari hasi zaidi kuliko habari chanya, hasa kutokana na ujio wa mitandao ya kijamii.
Amesema kuna umuhimu kwa waandishi wa habari na viongozi wa dini kubadilisha mtindo wa uandishi wa habari ili kusaidia kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii na kuepusha athari za habari hasi ambazo zinaathiri maadili ya vijana na jamii kwa ujumla.
Dk.Bulendu alikuwa mgeni rasmi,katika chakula kilichoandaliwa na BAKWATA Mkoa wa Mwanza, leo kwa ajili ya watoto yatima kutoka vituo 11 vilivyopo jijini humu, amehoji kwa nini watu wana chukiana, kwa nini nchi yetu imefika mahali mtu akifanya jambo jema wanaliacha na kutafuta mabaya,kwa nini mambo mema hayaendi.Upande wa dini mnayo majibu, sisi kwenye uandishi wa habari tuna majibu,”amesema.
Mhadhiri huyo wa Chuo cha SAUT amesema,utoaji habari wa aina hiyo unasababisha watu kutopendana,kukata tamaa, songo wa mawazo na sonona, ambapo habari kubwa zaidi zinazosumbua kwa sasa katika mitandao ya kijamii,ni za watu kuchukua uamuzi mgumu wa kukatisha uhai wao na kujiuliza kwa nini tumefika hapa.
“Ni kwa sababu ya habari tunazoilisha jamii zinawafanya wawe wakatili zaidi,watu kukata tamaa na kutokuipenda nchi yao,ipo haja ya kubadilisha aina habari na uandishi ili kujenga kizazi chema tuwasaidie viongozi wa dini,isifike mahala wanatuletea watoto wenye maadili tunawaharibu kwa habari zetu tunazowalisha,”amesema.
Dk. Bulendu, kwa niaba ya waandishi wa habari,amesema madhehebu ya dini yana vyombo vyao vya habari,hivyo tutapeana elimu ya namna bora ya kutengeneza maudhui yanayotakiwa na viongozi wa dini kwenye vyombo vyetu yatakayosaidia kujenga kizazi chema.
Amewasisitiza waandishi wa habari kama jamii,wanahitaji kubadilisha aina ya habari tunazozalisha ili kusaidia kujenga kizazi cha watu wenye maadili, huku akiwapongeza viongozi wa BAKAWATA kwa juhudi zao za kutunza watoto yatima.
Dk. Bulendu ameeleza kuwa kazi nzuri inayofanywa na vyombo vya habari vya kidini, ni muhimu vyombo vyote kuungana na kutoa elimu inayohamasisha maadili mema na kujenga jamii bora, vinapaswa kuchangia katika mchakato wa ujenzi wa jamii yenye umoja, upendo na maadili bora.
Amekumbusha kuwa dini, kusaidia yatima ni jambo la msingi na kwa mujibu wa Mtume Muhammad S.A.W, kusaidia yatima ni sawa na kutekeleza ibada nyingine muhimu kama kufunga na kusali usiku,ameshauri waandishi wa habari kuwa sehemu ya mabadiliko hayo kwa kutoa habari zitakazosaidia kupambana na ukatili na maovu dhidi ya watoto, ikiwa ni pamoja na yatima.
Kwa mujibu wa Dk.Bulendu palipo na madrasa nyingi kuna uwekezaji mkubwa maana yake kuna kizazi chenye maadili,ambapo kutokana na mahaba ya elimu nchini yanafanyika mapitio ya mitaala ili kutengeneza vijana wenye ujuzi zaidi waweze kumudu soko.
“Nimeona hapa watoto waliokusanyika wanapata elimu ya dini na elimu dunia (mazingira),Sheikh Kabeke ukiridhia wakati unatoa sadaka, yetu (waandishi wa habari) ya vifaa vya elimu,ije hapa iwasaidie watoto hawa kupata elimu ya dini na mazingira pia,kula chakula na yatima ni ibada, ni zaidi ya sadaka na moja ya nguzo za uislamu,”alieleza.
Amesema Sheikh Kabeke na BAKWATA waungwe mkono kwa miradi ya ujenzi wa vituo vya afya kupitia sera ya PPP ili kusaidiana na serikali kutoa huduma za kijamii kwa Watanzania.
Awali Sheikh Kabeke amesema kuwa kila mwaka wanaandaa chakula kwa ajili ya yatima wakishirikiana na Mkurugenzi wwa The Rocky Solution, Zakaria Nzuki,ambaye amekuwa akiunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,kwa kutoa mitungi ya gesi ya kupikia dhidi ya mapambano ya hewa ukaa .
“BAKWATA tunaongelea mustakabali wa nchi ,uchumi na maendeleo,tumeamua kuwa wazi ili kuondoa dhana ya upigaji ,tunajenga vituo vya afya ambapo Rais Samia ametuchangia sh. milioni 100, Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko sh.milioni Tano na Masanja Kadogosa, milioni kumi, hivyo bila amani, maji,barabara na umeme, havina maana na ndio sababu ya kuiombea nchi na Rais,”amesema.