Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Jenerali Patrick Nyamvumba akizungumza leo Aprili 03, 2025 na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam katika kuelekea kumbukizi ya miaka 31 tangu kutokea mauaji ya Kimbari nchini Rwanda. Kushoto ni Mratibu mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania, Susan Ngongi Namondo
Mratibu mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania, Susan Ngongi Namondo akizungumza na waandishi wa habari juu ya umoja wa Mataifa ambavyo utashirikina na Rwanda katika kumbukizi ya miaka 31 tangu kutokea mauaji ya Kimbari nchini Rwanda.
Na Avila Kakingo, Michuzi TV
IKIWA miaka 31 baada ya mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi, Rwanda imekuwa mfano wa ufanisi katika mchakato wa kujenga taifa linaloongozwa na mshikamano, maendeleo na utawala bora.
Nchi iliyoathiriwa vibaya na machafuko ya kivita, sasa inajivunia maendeleo makubwa, ikionyesha kasi ya ajabu katika kuimarisha uchumi, kuboresha huduma za afya, na kubuni mifumo ya usawa katika jamii.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Jenerali Patrick Nyamvumba wakati akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam. Amesema kwa wastani wa ukuaji wa uchumi wa asilimia 8 kwa mwaka tangu 1995, Rwanda imeweza kupunguza umaskini na kukuza sekta za afya, elimu, na miundombinu.
Umri wa kuishi umeongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka miaka 46.9 mwaka 2000 hadi 67.5 mwaka 2021. Aidha, Rwanda imejizatiti kuwa kinara wa usawa wa kijinsia, ambapo zaidi ya nusu ya majaji wa nchi ni wanawake.
Jenerali Nyamvumba amesema Rwanda pia imefanikiwa kuleta umoja wa kitaifa kwa kuondoa utambulisho wa kikabila katika vitambulisho vya raia, jambo lililosaidia kudumisha mshikamano na kupunguza mifarakano ya kijamii.
Hata hivyo, licha ya mafanikio haya, bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa, ikiwemo baadhi ya jitihada za kupotosha historia ya mauaji ya kimbari na kuendeleza itikadi za chuki. Aidha, hali ya usalama katika maeneo ya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inabaki kuwa tishio la amani ya kikanda, hasa kutokana na uwepo wa wanamgambo wa kikabila waliohusika na mauaji ya kimbari na ambao wanaendelea kutafuta kuanzisha machafuko.
MAADHIMISHO YA MIAKA 31 YA KUMBUKUMBU YA MAUAJI YA KIMBARI
Kwa Upande wa Mratibu mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania, Susan Ngongi Namondo amesema katika kuadhimisha miaka 31 ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari Jumatatu, Aprili 7, 2025, itakuwa ni siku muhimu kwa Wanyarwanda na jumuiya ya kimataifa, kwani wataadhimisha miaka 31 tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi. Maadhimisho hayo yatakuwa ya kipekee kwani yataadhimishwa katika balozi zote za Rwanda na ofisi za tume za ulimwenguni kote.
Na hapa nchini, Ubalozi wa Rwanda kwa kushirikiana na Mratibu mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania wameandaa hafla ya kumbukumbu itakayofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam siku hiyo hiyo ya Aprili 7, 2025 Vilevile, Arusha itakuwa mwenyeji wa maadhimisho mengine yatakayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), chini ya uratibu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika hafla hizi, shughuli kuu zitajumuisha kuweka mashada ya maua kwenye eneo la kumbukumbu ya mauaji ya kimbari mjini Arusha. Na kauli mbiu yake katika maadhimisho ya mwaka huu ni Tukumbuke- Tuungane- Tujijenge upya na ikihimiza maadhimisho ya kuunganisha Wanyarwanda na dunia, huku tukikumbuka yale yaliyopita na kujenga msingi thabiti kwa taifa lililo imara na lenye mshikamano.
Na neno “Kwibuka” linamaanisha “kukumbuka” kwa Kinyarwanda na linahusiana na lengo kuu la maadhimisho haya: kuheshimu kumbukumbu ya wahanga, kuwafariji manusura, na kuhakikisha kuwa mauaji ya kimbari hayajirudii tena.