Kamati ya Kudumu ya Bunge ya (PAC) imelipongeza Shirika la Nyumba la taifa (NHC), kwa utekelezaji mzuri wa ujenzi wa jengo la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika mji wa serikali Mtumba ambapo utekelezaji wake umefikia takribani asilimia 95.
Pongezi hizo zimetolewa leo Aprili 3,2025 hapa Jijini Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Japhet Asunga mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo hilo huku ikiitaka Wizara kumsimamia Mkandarasi ili kuhakikisha muda uliosalia anakamilisha ujenzi.
“Kuna maeneo machache ambayo hajayakamilisha, kuna baadhi ya kazi kazi tunataka azikamilishe mapema ili mwezi huu ukiisha basi Wizara iweze kuhamia hapa na kuanza kulitumia,”amesema.
Pia ameipongeza Serikali kwa fedha iliyotolewa takribani Bilioni 29 ili Wizara ya Ardhi iweze kupata ofisi za kisasa katika eneo hilo la Mtumba na wao kama kamati wameona zinatumika ipasavyo na mradi unatekelezwa kikamilifu kama ilivyokusudiwa.
“Leo tumeshuhudia ujenzi wa jengo unaendelea vizuri na liko katika viwango vizuri sana hivyo kamati yetu imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo hili na tumeipongeza Wizara kwa kusimamia vizuri pamoja na mkandarasi na mshauri mwelekezi kwa kufanya kazi vizuri, “amesema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amesema kuwa mradi ulikuwa utekelezwe ndani ya miezi 24 lakini kutokana na changamoto ya kuchelewa kukamilika na kuongezeka kwa gharama kutoka bilioni 24 mpaka 27 vimepelekea mradi kutokukamilika kwa wakati.
“Japo ukiangalia nasisi pia tulikuwa na changamoto zetu baadhi ya fungu zilikuwa zinachewa kwenda kwa mkandarasi lakini pia ukiangalia mfano kwenye mifumo ya moto ilikuwa imewekwa ya kizamani tukasema hapana inabidi iwekwe ya kisasa pamoja na uwekaji wa mifumo ya tehama,”amesema.
Naye mshauri Meneja wa miradi kutoka NHC Mhandisi Peter Mwaisabula ameipongeza kamati ya PAC kwa kutembelea mradi huo na kuongeza kuwa maelekezo yaliyotolewa wanaahidi kama wakandarasi kwa niaba ya menejimenti ya bodi watakwenda kuyatekeleza ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
Meneja wa mradi kutoka Wakala wa majengo Tanzania (TBA), Mbunifu Ng’olo Weja, amesema wao kama wasimamizi wa shughuli zote zinazotekelezwa na mkandarasi watamsimamia ili waweze kutimiza hazma ya kamati ya Bunge kwamba mkataba unapoisha na mshitiri aweze kuhamia kwenye jengo lake.











