Na Karama Kenyunko, Michuzi Blog.
SERIKALI ya Sweden na Tanzania zimesaini mkataba wa miaka mitano kwa lengo la kuwezesha tafiti za mabadiliko ya tabia nchi, kuimarisha mifumo ya ubunifu na mawasiliano ya sayansi kwa vyuo vikuu na kuimarisha mawasiliano ya kisayansi.
Mkataba huo wa miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2029, Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) itapokea Sh bilioni 10 kati ya hizo Sh bilioni 8.2 zitaingia Tanzania na fedha iliyobaki itakwenda kwa washirika wao wa Sweden ambao watahusika kutoa mafunzo katika masuala ya utafiti, ubunifu na mawasiliano.
Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo leo, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu amesema mazingira wezeshi waliyowekwa na serikali yamechangia wadau wa maendeleo kuendelea kuamini taasisi hiyo na kuwapatia fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi.
Amesema hiyo ni mara ya nne kwa Costech na Sweden kusaini makubaliano hayo na kwamba kwa kipindi chote cha ushirikiano, ilidhamini miradi 53 ya utafiti na ubunifu katika viwanda, bioteknolojia, uvuvi, kilimo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, maji, ufugaji na afya.
‘’Wafanyakazi 73 wa Costech walipata mafunzo ya usimamizi wa utafiti, fedha za utafiti, mawasiliano ya utafiti, ubunifu kwa maendeleo ya uchumi, mfumo wa usimamizi ubora, usimamizi wa fehda na haki miliki,’’ ameeleza Dk Nungu.
Dk Nungu amesema kupitia Sweden iliwasaidia kupata fedha kutoka Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) waliofadhili tafiti 40 za mabadiliko ya tabia nchi.
‘’Kwenye kongamano sayansi, teknolojia na ubunifu (STiCE) mwaka 2024, tulitoa hundi ya Sh bilioni 6.3 kwa ajili ya watafiti 19 wa mabadiliko ya tabia nchi na wengine tuliwaahidi tutawapatia, kupitia fedha hizi, watafiti 21 waliosalia watapatiwa fedha kwa ajili ya kukamilisha tafiti zao,’’ ameeleza.
Amesema Tanzania ina mifumo mizuri ya utafiti waliyojifunza kutoka nchini Sweden na kwamba taasisi nyingine za Afrika zinajifunza kupitia mfumo huo.
‘’Ghana, Sierra Leone , Cote d’Ivoire wamekuja kujifunza kwetu namna mfumo wetu unafanya kazi, tunajivunia hili na tunaahidi kufanikisha mkataba huu kukidhi mahitaji yaliyowekwa,’’ amesisitiza.
Kwa upande wake, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Macias, amesema msaada huo unalenga kuimarisha uwezo endelevu wa watafiti vyuoni, maendeleo ya miundombinu ya utafiti, na kuanzisha mifumo ya usimamizi wa utafiti.
‘’Licha ya changamoto ya Uviko 19, Costech katika miradi iliyopita ilifanikiwa kutengeneza mfumo wa kitaifa wa utafiti baada ya udaktari na kuwezesha watafiti kuandaa machapisho sita na bidhaa mbili ambazo ni vitafunwa vya afya kwa watoto na aina bora ya samaki aina ya tilapia, kusaidia miradi 24 ya utafiti iliyozalisha matokeo chanya katika mazingira, teknolojia bora ya uvuvi na chanjo ya mbuzi,’’ amefafanua Macias.
Amesisitiza katika mkataba huo, wataimarisha mifumo ya ubunifu na mawasiliano ya sayansi kwa vyuo vikuu vya Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Costech, kuimarisha mawasiliano ya kisayansi,’’ alisema.