Waziri wa Maji ,Nishati na Madini Mhe Shaibu Hassan Kaduara amesema Serikali inathamini michango iliyotolewa na waasisi na wanamapinduzi katika kuipigania Nchi
Akizungumza kwa niaba ya waziri Kaduara Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Sururu Juma Sururu ameyasema hayo huko Kinduni Wilaya ya Kaskazini B’ wakati wa Dua ya kumuombea muasisi wa Mapinduzi Marehemu Hafidh Suleiman Almas ikiwa ni wiki ya mashujaa.
Amesema kuwa wanamapinduzi hao walikua na umoja, usiri pamoja na nia thabiti katika kulipambania taifa na kuwa huru kwa wananchi wake.
“Wanamapinduzi wetu hawa walikua na umoja na nia thabiti katika kukomboa taifa hivyo na sisi tuwe vigezo kwa haya walioyafanya viongozi wetu na tuwaombee Dua” alisema
Mapema Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Hassan Abdalla Rashid amesema kuwa utaratibu uliyoanzishwa na Serikali ya awamu ya nane ya kuwaombea Dua waasisi hao ni mzuri hivyo ni vyema wananchi kuunga mkono utaratibu huo kwani ndio mustakabali mwema kwa maiti.
Akitoa neno la Shukurani mtoto wa marehemu Farhan Hafidh Suleiman ameishukuru Serikali kwa mchango wao na kuiomba Serikali kuendeleza utaratibu huo kwani inawapa faraja.



