
Jamii imetakiwa kutowaficha ndani watoto wenye ulemavu, kwani nao wana haki ya kupata elimu na malezi bora yatakayowasaidia kujitegemea katika maisha yao ya baadaye.
Wito huo umetolewa na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kalangalala, Rahima Yusufu, wakati wa shughuli fupi ya kukabidhi msaada wa vifaa mbalimbali kwa watoto wenye ulemavu katika Shule ya Msingi Mbungani, Manispaa ya Geita. Hafla hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Juma la Wazazi wa chama hicho.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Melle Mpangalala, amesema wameguswa na juhudi za kuhakikisha watoto hao hawatengwi, bali wanathaminiwa kama sehemu muhimu ya jamii.
Mkuu wa Shule ya Msingi Mbungani, Edith Ndunguru, ameeleza kuwa licha ya msaada waliopata, bado kuna mahitaji muhimu yanayohitajika ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto hao.
Nao wanafunzi wa shule hiyo wametoa shukrani zao kwa msaada waliopokea, wakisema utawasaidia katika masomo yao, huku wakiwaomba wasamaria wengine kuwakumbuka na kuendelea kuwasaidia.
Wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla wamehimizwa kuendelea kuwaunga mkono watoto wenye ulemavu kwa kuhakikisha wanapata haki zao za msingi, ikiwemo elimu na malezi bora. Aidha, imeelezwa kuwa mchango wa wadau mbalimbali ni muhimu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuimarisha mustakabali wa watoto hawa, ili waweze kufikia ndoto zao na kuchangia maendeleo ya taifa.