Naibu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Prof. Omary Swalehe akizungumza jambo wakati akifungua mafunzo ya usawa kijinsia katika masuala ya uongozi na biashara yalioratibiwa na Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa Ndaki ya Dar es Salaam, Kituo Cha Tegeta yaliofanyika leo April 4, 2025 , Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)

Balozi wa Norway Nchini, Mhe. Tone Tinnes akizungumza jambo katika mafunzo ya usawa kijinsia katika masuala ya uongozi na biashara yalioratibiwa na Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa Ndaki ya Dar es Salaam, Kituo Cha Tegeta

Meneja wa Kitengo cha Ubunifu, Ujasiriamali na Ushirikiano wa kitasnia Chuo Kikuu Mzumbe Profesa Emmanuel Chao akitoa mada katika mafunzo ya usawa kijinsia katika masuala ya uongozi na biashara yalioratibiwa na Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa Ndaki ya Dar es Salaam, Kituo Cha Tegeta.


Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) Bi. Imelda Lutebinga (kushoto) akijadili jambo na wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Kituo cha Tegeta.

Mkurugenzi wa Tanzania Startup Association Bw. Zahoro Muhaji akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Kituo cha Tegeta namna ya kufanikiwa katika ujasiriamali.


Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Kituo cha Tegeta wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ubalozi wa Norway nchini Tanzania, Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) pamoja na Taasisi za kibiashara nchini Norway (NHO)





………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania wametoa mafunzo ya usawa kijinsia katika masuala ya uongozi na biashara kwa wanafunzi wa Chuo hicho, Ndaki ya Dar es Salaam Kituo Cha Tegeta ambapo mafunzo haya ni sehemu ya juhudi na mpango mkakati wa kuwajengea uwezo ili waweze kujimudu katika nyanja mbalimbali na kufikia malengo yao.
Katika mafunzo hayo watoa mada wametoka Taasisi za kibiashara nchini Norway (NHO), Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), pamoja na Taasisi ya Startup Association Tanzania ambapo wamesisitiza umuhimu wa wanafunzi kuwa na subira pamoja na kutengeneza mahusiano wadau ili kufikia fursa kwa haraka.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo leo April 4, 2025, katika Kituo Cha Tegeta, Naibu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Prof. Omary Swalehe, amesema kuwa mafunzo yatawasaidia wanafunzi kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.
Naye, Balozi wa Norway Nchini, Mhe. Tone Tinnes, amesema kuwa lengo kuu la mafunzo haya ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata ujuzi utakaowawezesha kupiga hatua katika maisha na kazi zao.
Meneja wa Kitengo cha Ubunifu, Ujasiriamali na Ushirikiano wa kitasnia Chuo Kikuu Mzumbe Profesa Emmanuel Chao, amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mipango mikakati kuunganisha chuo pamoja na taasisi za nje ya chuo Kikuu Mzumbe katika kuleta elimu shirikishi.
Profesa Chao amesema kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo wanafunzi katika masuala ya uongozi unaozingatia uwasa wa kijinsia mahali pa kazi pamoja na shughuli za kijamii katika taasisi za umma na sekta binafsi.
“Wanafunzi wengi wanaotoka vyuoni wanakwenda kufanya kazi katika taasisi za umma na sekta binafsi, hivyo wasipoandaliwa vizuri wanaweza kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa” amesema Profesa Chao.
Amesema kuwa mafunzo yamegusa maeneo tofauti ikiwemo namna bora ya kuanzisha biashara pamoja na kutoa fursa kwa kuwapa nyenzo muhimu wanafunzi ili wanapomaliza chuo wajue wanafanya nini ili kufikia malengo.
Profesa Chao amesisitiza umuhimu wa jamii kuwa na utamaduni wa kujiendeleza kielimu pamoja na kujifunza kwa kutumia fursa ya mitandao ya kijamii jambo ambalo litasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) Bi. Imelda Lutebinga, amesema kuwa ni muhimu kuwapa elimu wanafunzi kwani ni sehemu ya kupanda mbegu, huku akieleza kuwa ATE imekuwa iendesha programu ya kuwajengea uwezo wanawake kulingana na uhitaji hasa katika nafasi ya uongozi.
Lutebinga amesema kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kutoa elimu kwa wahitimu zaidi ya 612 katika serikali ya Tanzania na Mapinduzi ya Zanzibar.
“Tulikuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe miaka 15 iliyopita na sasa tupo katika uchangiaji wa Nchi katika sekta mbalimbali pamoja na kushiriki katika nafasi ya maamuzi ili kusaidia kuendeleza dira ya Taifa” amesema Lutebinga.
Amesema kuwa wameendelea kutoa programu ya kutoa elimu ya kujiami, kujieleza kwa ufasaha ili kuhakikisha wanawake wanakuwa na uwezo kuongeza katika nafasi yoyote ya uongozi.
Nae, Mkurugenzi wa Tanzania Startup Association Bw. Zahoro Muhaji, amewataka wanafunzi kuwa wavumilivu, mawazo mazuri ya ujasiriamali pamoja na kutafuta mahusiano ya kibiashara kwa wawekezaji na watoa mitaji.
Bw. Muhaji amesema kuwa mahusiano na wadau mbalimbali wakiwemo wanasheria ni mbinu muhimu kwani ni fursa ya kupata wawekezaji pamoja na wateja.
Kwa upande wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Kituo Cha Tegeta wametoa shukrani kwa kupata mafunzo, kwani yamewasaidia kujifunza mbinu bora za kuanzisha na kuendesha biashara pamoja na uongozi ambazo zitawasaidia kuwa viongozi bora katika jamii na maeneo ya kazi.