Na Prisca Libaga Arusha
Katika jitihada za kuimarisha mazingira ya biashara na kukuza shughuli za ujasiriamali nchini, taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT) imezindua mtandao wa kuwaunganisha wafanyabiashara na fursa
mbalimbali za kiuchumi ndani na nje ya nchi.
Mtandao huo unaojulikana kama KLI Alumni Connect utawahusisha zaidi ya
wafanyabiashara 300 waliopitia programu za uongozi wa Biashara na ujasiriamali katika kipindi cha miaka mitatu kilichoendeshwa na KLNT kwa kushirikiana na chuo kikuu cha Regent kilichoko nchini Marekani.
Mafunzo hayo yanayoendeshwa chini ya kituo cha kibiashara cha Business Development center (BDC) Tanzania cha hapa nchini wajasiriamali kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma and Arusha wamenufaika.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo jana jijini Arusha,Mwenyekiti Mtendaji wa KLNT, Isaac Mpatwa amesema mtandao huo unalenga kuunganisha wahitimu wa programu hizo na fursa mbalimbali zinazowawezesha kukuza na kuimarisha biashara zao.
“Kupitia KLI Alumni Connect, tunawapa wahitimu wetu fursa ya kuunganishwa na ekosistemu ya biashara, mabenki, taasisi za maendeleo ya teknolojia, na wadau wa ndani na nje ya nchi kwa zaidi ya mataifa 100 duniani tulizo na mahusiano nazo”.
Amesema hiyo itawawezesha kupata Elimu zaidi, mitaji, ubunifu, teknolojia, vifaa, na masoko ya kimataifa.
Amesema mafunzo hayo yanaenda sambamba na safari katika nchi mbalimbali duniani .
“Hivi karibuni yenyewe tunatarajia kuhudhuria jukwaa la Biashara na uwekezaji linalojulikana kama ‘Tanzania-Israel Business and Investment
Forum [TIBIF] ’litakalofanyika kuanzia juni 8 hadi 14, 2025 Tel Aviv.
Jukwaa hilo muhimu la Biashara na uwekezaji, Mpatwa amesema kuwa wameandaa kwa lengo la kuwaleta pamoja wafanyabiashara wa Tanzania na Israel kwa madhumuni ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.
“Tunawapeleka wafanyakabiashara wetu nchini Israel ili kuwaunganisha na masoko, miradi, mitaji, fedha, mafunzo, na ushauri wa kibiashara katika sekta mbalimbali kama elimu, ufugaji, uvuvi, viwanda, teknolojia na utalii” amesema na kuongeza
“ Tunataka wafanyabiashara wetu wapate nafasi ya kukutana na wenzao wa Israel kupitia mikutano midogo midogo ya kibiashara ‘Business to business Meeting[B2B]’ iliwaweze kufaidika na fursa za biashara zinazofanana na wenzao”
Mpatwa amesema kuwa hayo yote yanafanyika kwa ushirikiano na serikali chini ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Wizara ya Viwanda na
Biashara, Wizara ya Uwekezaji, na Wizara ya Mambo ya Nje.
“Ushirikiano huu unalenga kubadilishana maarifa, miradi, na uzoefu kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuhakikisha wafanyabiashara wetu wanaungwa mkono na mifumo rasmi ya kiuchumi na unatoa fursa za kufanikisha makubaliano ya kibiashara kati ya wafanyabiashara na serikali, au serikali za nchi washirika na nchi yetu.
Mmoja wa wafanyabiashara wahitimu katika programme hiyo, Rephrine Kombe amesema mafunzo hayo ya wiki 20 yamewasaidia kuwapa ujasiri wa kuwasilisha mawazo yao na kuboreshwa na wataalamu hao wa biashara na
kuwasaidia kuanza safari rasmi ya kibiashara.
“Mimi nilikuwa na wazo tayari, hivyo nikasaidiwa kuboresha nawakufunzi wetu ambao ni maprofesa wa biashara, na sasa nimefanikiwa
kuwa na biashara halisi, na zaidi nimefanikiwa kuingia kwenye mfumo rasmi wa kiserikali” amesema Rephrine ambae ni Mkurugenzi wa kiwanda cha kutengeneza taulo za kike cha Reepads’ .
Aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Programe hiyo, Meya wa jiji la Arusha Maximmilian Iranghe amesema kuwa elimu hiyo ya ujasiriamali
ya vitendo ni nzuri ambayo inasaidia pia serikali kukuza ajira na kukua kiuchumi kwa jamii.
“Kadri wananchi wake wanavyokua na uchumi mzuri ndivyo na serikali
inavyozidi kukua hivyo niwapongeze sana KLNT na niseme kuwa serikali
itaendelea kuwaunga mkono wafanyabiashara na wajasiriamali wote nchini
hasa katika kutatua changamoto zao wanazokumbana nazo ili kukuza biashara zao”.

