Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa Mahakama, hususan Mahakama za Mwanzo kutokufungwa na masharti ya kiufundi katika utoaji haki ili kurahisisha upatikanaji wa haki na kuzidi kujenga imani kwa wananchi kuwa Mahakama ndio kimbilio lao kuu katika kudai haki.
Rais Dkt. Samia amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania uliyofanyika katika eneo la Tambukareli, jijini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Sharifa B. Nyanga imesema Rais Dkt. Samia amesisitiza umuhimu wa jengo hilo lililogharimu Shilingi Bilioni 129.7 kutunzwa na kutumika ipasavyo na umuhimu wa ubora wa huduma zinazotolewa kuendana na ubora wa uwekezaji uliofanywa kwenye jengo hilo.
Sambamba na hilo, Rais Dkt. Samia amezindua miradi mingine miwili ikiwemo jengo jipya la ghorofa sita la Tume ya Utumishi wa Mahakama, pamoja na nyumba 48 za kisasa za makazi ya Majaji zilizopo jijini Dodoma.
Aidha, katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wote na kwa wakati, Rais Dkt. Samia alieleza haja ya Mahakama ya Tanzania kuendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika kutoa huduma za kimahakama ili kuendana na kasi ya dunia, kurahisisha uendeshaji wa mashauri na upatikanaji haki.
Rais Dkt. Samia pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha Mahakama Maalum zinazoshughulikia masuala ya ardhi, familia na biashara ili nazo zitoe huduma bora na kuchangia ukuaji wa sheria kwenye maeneo yao.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amepongeza utendaji kazi wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma kwa kuitumikia nafasi hiyo kwa ufanisi na uzalendo na kuleta maboresho makubwa kwenye Mahakama.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 104 ya uwepo wake, Mahakama ya Tanzania sasa ina Makao Makuu yenye hadhi. Aidha kwa Mahakama ya Tanzania kuhamia rasmi Mkoani Dodoma kunafanya mihimili yote mitatu ya Serikali kuwepo makao makuu ya nchi.