Na: Mwandishi Maalumu – Dodoma
05/04/2025 Imeelezwa kuwa ukuaji na maendeleo ya Teknolojia umechochea kwa kiwango kikubwa katika ufanisi wa kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo hapa nchini.
Hayo yamebainishwa jana Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya wakati akitoa wasilisho kwenye mdahalo wa Kitaaluma (Symposium) uliofanyika wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa.
Dkt. Angela alisema matumizi ya Teknolojia yamekuwa na ufanisi mkubwa kwenye matibabu ya magonjwa ya moyo kwani kwa kutumia simu Janja App mwananchi anaweza kupima mapigo ya moyo, shinikizo la damu na umeme wa moyo.
“Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa wa kitaaluma na teknolojia katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, na sasa matibabu ya moyo yamejikita katika matumizi ya teknolojia ili kuongeza ufanisi na wigo wa huduma kwa kiwango kikubwa” alisema Dkt. Angela
Aidha, Dkt. Angela alibainisha kuwa magonjwa yasiyoambukiza bado ni tatizo kubwa duniani huku magonjwa hayo yakiendelea kuwa sababu inayoongoza kwa vifo vyote vinavyotokea kila mwaka.
“Takribani watu milioni 470 hugundulika kuwa na magonjwa ya moyo duniani na kati ya hao vifo vikiwa ni kwa watu milioni 17.6(3.9%) kwa mwaka, tatizo hilo tunaliona pia katika nchi za uchumi wa kati”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela alisema JKCI imeweza kufikia zaidi ya mikoa 16 hapa nchini na kutoa huduma ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyowafikia wananchi elfu ishirini (20,000) huku 42% ya wananchi kukutwa na magonjwa ya moyo.
“Baadhi ya mikoa tuliyoifikia ni pamoja na Tabora , Kilimanjaro, Geita, Dar es Salaam, Arusha, Mtwara, Lindi, Zanzibar, Dodoma, Iringa, Manyara na Pwani lengo letu ni kutoa elimu kwa wananchi ya namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo na kuwasaidia wale ambao tayari wameshakutana na changamoto za maradhi hayo”, alisema Dkt. Angela
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inashiriki katika maadhimisho ya wiki ya Afya Kitaifa yaliyoanza tarehe 3 hadi 8, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Jijini Dodoma yanayoenda sambamba na kaulimbiu “Tulipotoka, Tulipo, Tunapokwenda , Taifa Imara lenye Afya ”.