Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro imeadhimisha Wiki ya Afya kwa kufanya kikao na viongozi wa dini na wa kimila, ambapo wamehimizwa kutumia majukwaa yao kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya, lishe bora na mtindo wa maisha, ili kupambana na matokeo ya lishe duni.
Wito huo ulitolewa na Katibu Tawala Msaidizi wa Wilaya ya Same, Ndg. Sixbert Sylvester, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uhamasishaji wa Afua za Afya na Lishe kwa Viongozi wa Dini na Viongozi wa Kimila.
“Serikali ina imani kubwa na ninyi, tutakapounganisha nguvu na kuendelea kutumia fursa ya majukwaa yenu kuelimisha na kuhamasisha jamii, tutaweza kufikia adhma ya kuboresha afya na ustawi wa jamii kwa ujumla,” alisema Ndg. Sixbert Sylvester.
Katika hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa kuhamasisha utoaji wa chakula shuleni, upandaji wa miti, ufugaji wa kuku, na kilimo cha mbogamboga ili kupambana na changamoto za lishe duni katika jamii.
Akizungumzia malengo ya mafunzo hayo, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Bi. Yuster Malisa, alisema viongozi wa dini na wa kimila wanayo nafasi muhimu katika kufikisha ujumbe wa afya kwa jamii kubwa wanayoshirikiana nayo mara kwa mara. Mada zilizojadiliwa ni pamoja na lishe bora, mlo kamili, mtindo bora wa maisha, na magonjwa yasiyoambukiza.
Afisa Lishe wa Wilaya ya Same, Bi. Jackline Kilenga, alielezea changamoto kubwa ya lishe duni, ikiwa ni pamoja na udumavu kwa watoto na uzito kupita kiasi, akiongeza kuwa viongozi hawa wa dini na kimila wataweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya na lishe bora.