Na Sabiha Khamis Maelezo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Mhe. Ali Suleiman Ameir amesema hatua iliyochukuliwa na Serikali kuwaombea dua Viongozi na Waasisi wa Mapinduzi ni ishara ya kuendeleza umoja na mshikamano waliouacha waasisi hao.
Ameyasema hayo katika ziara ya kuomba dua katika kaburi la Kamishna wa Polisi Mstaafu Hayati Eddington Herbert Kissassi Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi B Unguja.
Aidha Mhe Ali amefahamisha kuwa Serikali licha ya kuwaombea dua bado inahakikisha inaendelea kuwaenzi, kuwatunza pamoja na kuthamini mawazo, michango ushauri na matendo yao mema ambayo wameifanyia Serikali katika kuitetea nchi.
Aidha ameitaka jamii kuendelea kuyatunza na kuyathamini mazuri ambayo yamefanywa na viongozi waliopita ili kuendelea kulinda amani ambayo imewezesha hivi sasa kuweza kujitawala wenyewe na kuwa na uhuru wa kujitafutia maendeleo.
Ameendelea kwa kusema kuwa mazuri hayo yanaendelea kutumika na kutoa muongozo katika maamuzi mbali mbali ya uwajibikaji wa majukumu ya kiserikali.
Hata hivyo amesisitiza umoja na mashirikiano katika kuonesha njia nzuri ili kuweza kukumbukwa na vizazi vijavyo kutokana na mazuri ambayo yataweza kuleta faida kwa nchi.
Kwa upande wao wanafamilia ya Hayati Eddington Herbert Kissassi wameishaukuru Serikali kwa kuwaenzi na kuthamini michango ya viongozi na waasisi wa Mapinduzi katika kupigania uhuru wa nchi.
Akisoma Misa takatifu Rev Canon. Christopher Barankera kutoka Kanisa la Anglican Zanzibar amesema kiongozi huyo ametumikia nchi kwa uaminifu pamoja na waasisi wengine ambao wamiepigania nchi kwa kuwaweka huru Wazanzibar.
Maadhimisho ya wiki ya kuwaenzi viongozi wa Kitaifa, Waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Katibu wa kwanza wa Chama cha Afro Shirazi ambapo kilele kitafanyika Aprili 7, 2025 Kisiwandui Wilaya ya Mjini, Unguja.