Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia kundi la G55 limesisitiza umuhimu wa kushiriki uchaguzi mkuu wa 2025 hata kama mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi hayatakuwa yamepatikana kwa wakati.
Wamesisitiza kuwa wataendelea kuunga mkono madai ya mabadiliko pamoja na madai ya kufanyika kwa reforms katika Nchi na wapo tayari kuongeza nguvu katika jitihada za chama ya kudai mabadiliko ya katiba pamoja mabadiliko ya sheria ili kuwa na uchaguzi huru na kuaminika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo April 6, 2025 Jijini Dar es Salaam, Aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA John Mrema, amesema kuwa
kwenye eneo la reforms watu waliogombea uchaguzi mwaka 2020 umewajeruhiwi kutokana na mifumo ya uchaguzi sio rafiki.
Mrema amesema kuwa wanaunga mkono asilimia 100 suala la reforms, huku akieleza kuwa wapo tayari kuongeza nguvu na kuwekeza kupigania mabadiliko ya mfumo na sheria kwa ajili ya uchaguzi huru na haki .
“Katika No election tumeona njia ambazo zimetumika sio sahihi, ndiyo maana tumechukua maamuzi ya kukishauri chama chetu, kwani hatuoni kama njia hiyo inaweza kutufikisha huko tunakotaka kwenda” amesema Mrema.
Mrema amesema kuwa hawawezi kuzuia uchaguzi wakiwa nje ya uchaguzi, kwani kufanya hivyo ni sawa na kufanya kosa la jinai, huku akifafanua kuwa njia pekee ya kuzuia uchaguzi ni kushiriki uchaguzi wenyewe kwa kuhakikisha wanaingiza wagombea katika uchaguzi.
“Ni rahisi wagombea kuhamasisha na kuongea wananchi kuzuia uchaguzi katika vituo mahususi katika Kata au Majimbo yanayotaka kufanyiwa hujuma” amesema Mrema.
Amesema dhana ya No Reforms No Election haikuwahi kumaanisha kususia au kuzuia uchaguzi, bali ilikuwa ni wito wa kuunganisha jamii katika kudai mageuzi ya mfumo wa uchaguzi.
“Dhana ya No Reforms No Election, tofauti nini wakati wa uenyekiti wa Mheshimiwa Freeman Mbowe
na sasa uenyekiti wa Tundu Lissu ?, nimeeleza tangu awali kwamba tunatofautiana kwenye dhana ya utekelezaji wa No Election. hakuna mahali kwenye nyaraka za chama ambapo imetafsiriwa kuwa No Election ni kususia au kuzuia uchaguzi,” amesema Mrema.
Amesisitiza kuwa msingi wa dhana hiyo ni kuunganisha makundi ya kijamii kwenda pamoja kushinikiza mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi nchini, na si kujitenga na mchakato wa uchaguzi kabisa.
“Dhana ya No Reforms No Election ilikuwa na lengo la kuunganisha makundi yote katika jamii, twende pamoja tukadai reforms. Ndiyo msingi wake huo, ni kuunganisha makundi ya kijamii kwenda kushinikiza mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi wa nchi,” ameongeza.
Hata hivyo amesikitishwa na ujumbe wa mwanaharakati Maria Sarungi aliyoandika katika mtandao wa X akikitaka CHADEMA kuweka hadharani majina ya watu wote wanaotaka ubunge bila Reforms, huku akisema kuwa ametuhumu kuwa watu hao wanataka kutishia kuhama Chama.
Amesema kuwa kauli hizo za Maria Sarungi ambaye siyo mwanachadema zinafanana za Mhe. Lissu na Mhe. Godbless Lema pamoja na kuingilia Mamlaka ya Chama, huku mwenyekiti Lissu akinyamaza kimya
“Mwanaharakati Sarungi anamaslahi yake ya kukitaka chama kutoshiriki uchaguzi wa mwaka huu” amesema Mrema.