Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Dk Khalid Salum Mohamed akitoa hotuba kuhusiana na Maisha ya aliekua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya Pili Sheikh Ali Hassan Mwinyi baada ya kumaliza kisomo cha Dua ya Khitma Kumuombea Kiongozi huyo hafla iliofayika katika Msikiti wa Mangapwani Kaskazini Unguja.Ikiwa ni muendelezo wa Wiki ya Kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa,Waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar.
Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Dk Khalid Salum Mohamed akitoa hotuba kuhusiana na Maisha ya aliekua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya Pili Sheikh Ali Hassan Mwinyi baada ya kumaliza kisomo cha Dua ya Khitma Kumuombea Kiongozi huyo hafla iliofayika katika Msikiti wa Mangapwani Kaskazini Unguja.Ikiwa ni katika Wiki ya Kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa,Waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar.
Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Dk Khalid Salum Mohamed(wanne kushoto)akiwa pamoja na Viongozi mbalimbali na Wananchi wakiomba Dua katika Kaburi la Aliekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya Pili Sheikh Ali Hassan Mwinyi aliezikwa Kijijini kwake Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja.Ikiwa ni katika Wiki ya Kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa,Waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar.
PICHA NA YUSSUF SIMAI, MAELEZO ZANZIBAR.
……………..
Na Rahma Khamis Maelezo
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dkt. Khalid Salum Mohamed amesema kuwa Marehemu Mzee Ali Hassan Mwinyi alikuwa kiongozi aliyependa mambo mema, hivyo kuna kila sababu ya kuendelea kumuenzi na kumkumbuka kwa mazuri aliyoyatenda wakati wa uhai wake.
“Nawaomba ndugu zangu na Waislamu wenzangu tuyafuate yale yote aliyoyafanya kwa maslahi ya taifa. Ni vyema, japo mara moja, tukakisoma kitabu alichokiandika Mzee huyu ili kunufaika na busara zake,” alisema Dkt. Khalid.
Kauli hiyo aliitoa huko Mangapwani, Wilaya ya Kaskazini B, wakati wa dua maalum ya kumuombea Marehemu Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema kuwa utamaduni wa kuwaombea dua viongozi waliotangulia ni utaratibu mzuri unaopaswa kuendelezwa, kwani viongozi hao walifanya kazi kubwa katika kuikomboa nchi, kudumisha amani na utulivu, pamoja na kuleta maendeleo.
Aidha, ameushukuru uongozi wa Awamu ya Nane kwa kuendeleza utamaduni huo wa kuwaombea dua viongozi waliotangulia na kuuhifadhi kama sehemu ya urithi wa taifa.
Dkt. Khalid aliongeza kuwa Mzee Mwinyi alikuwa mtu wa kupenda maendeleo, na alihimiza mambo mema kama vile upandaji wa miti ya matunda, elimu ya dini, na uchimbaji wa visima — ambayo yote ni miongoni mwa amali njema.
“Mtume Muhammad (SAW) amesema: ‘Mtu anapofariki, mambo yake yote hukatika isipokuwa matatu – sadaka endelevu, elimu yenye manufaa, na mtoto mwema anayemuombea dua.’” Alikumbusha Dkt. Khalid.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B, Mhe. Sururu Juma Sururu alisema kuwa utaratibu huu wa kuwaombea dua viongozi ni jambo jema kwani unakumbusha na kuenzi mazuri yaliyofanywa na viongozi waliotangulia.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya familia, Mzee Juma Mgeni Kombo ameishukuru Serikali kwa kuanzisha na kuendeleza utaratibu huo, na akapendekeza kuwa utamaduni huo uendelee hata kwa viongozi wengine watakaofuata.
Wiki ya mashujaa hufanyika kila ifikapo Aprili mosi Hadi Aprili 7 ambapo huadhimishwa kwa Dua kubwa inayotarajiwa kufanyika hapo kesho Ofisi Kuu Kisiwandui.