Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland anayehusika na Bara la Afrika, Mjini Warsaw nchini Poland, Mhe. Anna Radwan-Röhrenschef, ambapo wamejadiliana namna ya kuimarisha diplomasia ya uchumi kati ya nchi hizo mbili kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini Tanzania katika sekta za kilimo, ujenzi wa miundombinu ya Reli ya Kisasa ya SGR na kuangazia fursa nyingine ambazo Poland pamoja na sekta binafsi ya nchi hiyo wanaweza kuwekeza ikiwemo Sekta ya nishati, usafiri, maji, afya na mingine mingi.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akimkabidhi zawadi ya bidhaa zinazotengenezwa nchi Tanzania, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland anayehusika na Bara la Afrika, Mjini Warsaw nchini Poland, Mhe. Anna Radwan-Röhrenschef, baada ya kufanya kikao na kujadiliana namna ya kuimarisha diplomasia ya uchumi kati ya nchi hizo mbili kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini Tanzania katika sekta za kilimo, ujenzi wa miundombinu ya Reli ya Kisasa ya SGR na kuangazia fursa nyingine ambazo Poland pamoja na sekta binafsi ya nchi hiyo wanaweza kuwekeza ikiwemo Sekta ya nishati, usafiri, maji, afya na mingine mingi. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha, Warsaw, Poland.
…………
Na Benny Mwaipaja, Warsaw, Poland
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland anayehusika na Bara la Afrika, Mjini Warsaw nchini Poland, Mhe. Anna Radwan-Röhrenschef, ambapo wamejadiliana namna ya kuimarisha diplomasia ya uchumi kati ya nchi hizo mbili kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini Tanzania katika sekta za kilimo, ujenzi wa miundombinu ya Reli ya Kisasa ya SGR na kuangazia fursa nyingine ambazo Poland pamoja na sekta binafsi ya nchi hiyo wanaweza kuwekeza ikiwemo Sekta ya nishati, usafiri, maji, afya na mingine mingi.
“Tunapoendelea kuimarisha ushirikiano wetu wa muda mrefu, ninaialika Poland kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano yatakayoimarisha zaidi uhusiano wetu na kuimarisha zaidi uchumi wa Mataifa yetu mawili pamoja na watu wetu katika nyanja za ujenzi wa miundombinu ya maji, nishati, barabara, hususan katika Jiji letu la Dodoma ambalo idadi kubwa ya watu inazidi kuongezeka na kuhitaji huduma hizo muhimu” alisema Mhe. Dkt. Nchemba.
Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba alitoa rai kwa Poland kuisaidia Tanzania kuongeza ujuzi wa kiufundi kwa watanzania hususan vijana kupitia mafunzo maalumu ya ufundi na kutoa nafasi za masomo ama mafunzo ya juu kwa wataalam wa kitanzania ili kuwaongezea ubobezi katika taaluma zao kwa manufaa ya nchi, katika maeneo mahsusi ya fedha, teknolojia, na mapinduzi ya viwanda hali itakayochangia mageuzi makubwa ya kiuchumi yanayofanyika nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland anayehusika na Bara la Afrika, Mhe. Anna Radwan-Röhrenschef, alisifu ushirikiano imara uliopo katı ya nchi yake na Tanzania na kuahidi kuendeleza uhusiano huo kwa kuchangia ujenzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini humo kwa faida ya nchi hizo mbili.
Alimpongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo SGR, pamoja na kusimamia vizuri uchumi wa nchi ambao umekuwa imara kwa kusimamiwa vyema na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye ni msaidizi wake.
Alisema kuwa nchi yake inatamani kujifunza kutoka Tanzania kwa kuwa licha ya Taifa lake kuwa kubwa kiuchumi, lakini uchumi wake umepata changamoto katika kipindi hiki cha mzozo wa vita vya Ukraine na Urusi, pamoja na athari za UVIKO-19.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Poland, Mhe. Hassani Iddi Mwamweta.



