NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ambayo itafanyika Aprili 13,2025 kwenye ukumbi wa The Super Dome Masaki Jijini Dar es Salaam..
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 7, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, Prof. Penina Mlama amesema vigezo vilivyotakiwa kutumika katika kushiriki kushindania Tuzo hiyo vilitangazwa kna pia mwitikio mwaka huu ni kama ilivyokuwa miaka miwili ya nyuma, umekuwa mzuri.
Amesema Tuzo hiyo kwa Mwaka huu wa 2024 /25 inahusisha nyanja nne za ushairi, riwaya, hadithi za watoto na tamthiliya.
“Utaratibu wa zawadi kwa washindi utabaki kama ilivyokuwa miaka iliyopita yaani, Mshindi wa kwanza Shilingi milioni 10, Muswada wake utachapishwa na serikali na kusambazwa shuleni na maktaba za taifa, Ngao na Cheti. Mshindi wa Pili atapata Shilingi milioni 7 na Cheti, pia Mshindi wa tatu nae atapata Shilingi milioni 5 na Cheti”. Ameeleza Prof. Mlama.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa serikali inataka kuhamasisha utamaduni wa kusoma vitabu nchini ndio maana wanaelea kuhamasisha watu waweze kutenga muda wa kujisomea vitabu.
“Watanzania wengi hawana utaratibu wa kujisomea vitabu, hivyo tunaamini kwa kutumia waandishi wetu nchini wataweza kuandika vitabu na kuhamasisha watu kusoma vitabu”. Amesema Prof. Mkenda.
Amesema kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa mwandishi mzuri aliweza kuandika vitabu mbalimbali na namna amechangia kukuza lugha ya kiswahili hivyo kumuenzi kwake wameamua siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake kuwepo kwa utoaji wa tuzo hizo.