Katika Kongamano la 8 linaloendelea la Uongozi la Afrika (ALF), viongozi hao wamehimiza matumizi ya fursa hiyo na kuweka mazingira mapya yatakayowezesha ‘Afrika Kwanza’ katika juhudi za kutimiza Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs).
Wito huo ulitolewa siku ya Jumatatu katika kongamano la ALF lililofanyika Kampala, nchini Uganda na lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi wa Afrika kwa Maendeleo Endelevu (Taasisi ya UONGOZI) likiwa na kauli mbiu ya, “Kutekeleza Malengo Endelevu ya Maendeleo Barani Afrika: Maendeleo na njia ifuatayo”.
SDGs, ambazo zimetokana na wito wa kimataifa wa kuchukua hatua zinazolenga kutokomeza umaskini, kulinda mazingira, na kuhakikisha ustawi kwa wote, ziliasisiwa tangu mwaka 2015. Kongamano hilo linaloendelea linajadili hali ya sasa ya utekelezaji wa SDGs katika nchi za Afrika huku likibaini changamoto kuu na vikwazo vinavyozuia maendeleo.
Akifungua Kongamano hilo, Rais wa Uganda Yoweri Museveni alirejelea SDGs kwa kuzivunjavunja kama zilizoelekezwa katika kuondoa vikwazo vya kimkakati vinavyozuia mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika bara la Afrika.
Alibainisha kuwa ili nchi zielekee kwenye mabadiliko, zinapaswa kuanzia katika ngazi ya chini ya kujenga nchi imara zenye uwezo na sera nzuri zinazozingatia maslahi ya kitaifa. Kwa upande wa nchi yake, alisema uchumi wao umejengwa katika hatua 5 tangu walipoanza kuendesha serikali, kwa namna ya kurejesha kidogo, kupanua uchumi wa zamani wa kikoloni, kubadilisha uchumi, kuongeza thamani kwenye uchumi na kuelekea kwenye uchumi wa maarifa.
Akiweka muktadha wa kongamano hilo, Mratibu wa ALF 2025, ambaye pia ni Mlezi wa ALF na Rais wa Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alibainisha kuwa katika kurekebisha utekelezaji wa SDGs kwenye njia sahihi, uharaka wa hatua hauwezi kupuuzwa pamoja na utashi wa kisiasa wa hali ya juu na kubadilisha matarajio kuwa matendo.
Alisema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto katika utekelezaji, zinapaswa kugeuzwa kuwa fursa na kuthibitisha tena dhamira ya ndani kwa SDGs na Ajenda ya Afrika 2030.
Pia alitoa wito wa kupewa kipaumbele kwa ukuaji wa uchumi ambao huzaa ajira na elimu inayoweza kuleta matokeo ya kujifunza ya kiwango cha dunia na daraja la kati.
Naye Mratibu Msaidizi wa ALF na Waziri Mkuu wa Zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn alibainisha kuwa Afrika inakabiliwa na fursa lakini pia changamoto katika kufikia malengo ya SGDs, kama vile uhaba mkubwa wa ufadhili na hivyo rasilimali kubwa zinahitajika kuziba pengo hilo.
Pia alipendekeza njia mbadala za kufadhili SDGs lakini wakati huo huo akitoa wito wa kuimarishwa kwa utawala na taasisi, uwazi, utawala wa sheria, kupambana na rushwa na kuzuia mianya haramu ya fedha. Hili, linapaswa kwenda sambamba na nguvu kazi imara, uhakika endelevu wa chakula, nishati ya uhakika na kuimarisha ushirikiano katika biashara na uchumi mpana katika bara lote kwa kukubali kupunguziwa kwa uhuru wa nchi binafsi na kukumbatia Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA), alisema.
“Kama inakuwa vigumu kufanya biashara na uchumi ulioimarika zaidi wa magharibi, ni vyema kuimarisha biashara za ndani, kutumia teknolojia na uvumbuzi, kuhamasisha rasilimali na kupunguza misaada ya kigeni na Misaada Rasmi ya Maendeleo (ODA).” Aliongeza.
Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa ya Afrika, Antonio Pedro alibainisha kuwa katika utekelezaji wa SDGs, ni muhimu kuelewa kuwa ukosefu wa ajira si suala la kiuchumi tu bali pia ni tishio kwa amani na jaribio kwa mfumo wetu wa kiuchumi, akiongeza kuwa sekta binafsi haipaswi kuwekeza tu kwa faida bali pia kwa lengo.
Alisema kuwa bara lilihitaji mfumo mpya wa SDGs, akibainisha zaidi kuwa kuondoa vikwazo vya ushuru na visivyo vya ushuru kuna uwezo wa kuongeza biashara ya ndani ya Afrika kwa asilimia 45 katika muongo ujao na kwamba wakati uchumi wa kimataifa wa Akili Mnembe unatarajiwa kufikia dola trilioni 1.8 ifikapo mwaka 2030, huku Afrika ikiwa bado na asilimia 1 tu ya hiyo.
Katika taarifa muhimu, Mwakilishi wa Zamani wa FAO nchini Ethiopia, Umoja wa Afrika na UNECA, Mratibu Mkuu wa FAO kwa Afrika Mashariki, Bw. Mafa Chipeta, alisisitiza mbinu ambayo ni chaguo bora zaidi na iliyolenga upya katika utekelezaji, akibainisha kuwa ikiwa bara litachukua SDGs zote kwa mara moja, linaweza kujiminya sana.
Msingi wa hoja yake ulihusishwa na ukweli kwamba bara la Afrika lina asilimia 17 hadi 18 ya idadi ya watu duniani lakini likiwa na asilimia 2 tu ya Pato la Taifa la Dunia na biashara, likiwa na alama ya asilimia 3 kwa viashiria vingi vya kiuchumi na likiwa na chini ya asilimia 0.5 tu kwa teknolojia mpya muhimu.
Alionya zaidi kuwa wizara za biashara za Afrika zina utamaduni wa kupuuza biashara kubwa ya ndani kuliko biashara ya nje ambayo inawaacha wafanyabiashara wanyonyaji kuwaibia wakulima wadogo na inaendelea kutoa ruzuku kubwa kwa uchumi wa dunia kwa kuuza malighafi, ambayo haijasindikwa na yenye thamani ndogo kwa bei rahisi na kuja kununua tena bidhaa kwa bei za juu.
Alipendekeza kuwa bara linahitaji kupunguza utegemezi kutoka wafadhili kwa kutenga fedha zake ili wafadhili wasiwe mbadala wa nafasi ya dhamira ya ndani.
Rais wa Zamani wa Jamhuri ya Sierra Leone, Dkt. Ernest Bai Koroma, alibainisha kuwa wakati mpango wa sasa wa ‘Amerika Kwanza’ umeleta hali ya sintofahamu katika sehemu nyingi za dunia, ilikuwa ni muda muafaka kwa Afrika kutumia fursa hii ili iweze kujipanga upya na kufanya maamuzi mapya ya ujasiri katika mwelekeo mpya wa maendeleo.
Alihimiza kutoa kipaumbele katika maendeleo ya rasilimali watu kupitia elimu, afya na utoaji wa huduma za kijamii, maendeleo ya kilimo na utawala bora wenye uongozi uliodhamiria kuendesha michakato yote hii.
Naye Rais wa Zamani wa Jamhuri ya Tunisia Dkt. Mohamed Moncef Marzouki alitoa wito kwa Afrika kujitegemea kupitia biashara ya ndaniya wao kwa wao, ambazo zinapaswa kutanguliwa kwa kuwa na serikali za kidemokrasia, huru na zisizojihusisha na rushwa.
Naye Makamu wa Rais wa Zamani wa Uganda, Gilbert Bukenya, alisema Afrika inapaswa kuwa na uongozi bunifu ambao utawakwepa wale wanaotaka kuiendesha kwa maslahi ya nje na badala yake kuendesha ajenda yake yenyewe ya mabadiliko.
Waziri Mstaafu wa Mambo ya Nje, Sam Kutesa, alisema SDGs zilikuwa matarajio sahihi na kwamba kilichohitajika kwa bara hili ni kubuni hatua mpya za kufadhili utekelezaji wake, kama vile kutumia rasilimali asili za ndani na ufadhili kutoka sekta binafsi.
Kongamano hili limejumuisha vikao vinne vya mada kuhusu kutokomeza umaskini na ukuaji wa uchumi, afya na ustawi, elimu na maendeleo ya ujuzi; na uendelevu wa mazingira na hatua za tabia nchi.
Kongamano hili ni tukio muhimu linalotangulia Mkutano wa 11 wa Kikanda cha Afrika kuhusu Maendeleo Endelevu ya Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA), ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 9 – 11 Aprili 2025.
Taasisi ya Uongozi wa Afrika kwa Maendeleo Endelevu, ijulikanayo kama TAASISI ya UONGOZI, ni kituo cha kikanda cha maendeleo ya uongozi kinachofanya kazi chini ya Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2010 na Serikali za Tanzania na Finland, inajikita katika kuhamasisha na kuwawezesha viongozi wa Afrika kutoa suluhisho jumuishi na endelevu katika mataifa yao na bara la Afrikakwa ujumla