Na: Calvin Gwabara – Mwanza.
Baraza la Kiswahili la Taifa
(BAKITA) lapongeza kazi kubwa inayofanywa na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria
kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya kuhakikisha sheria zote za
Tanzania zinaandikwa kwa lugha mama ya Kiswahili.
Mhariri Mkuu wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) bwana Richard Ntambi akitoa salamu za baraza hilo mbele ya Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini (hayupo pichani) |
Akizungumza na Waandishi wa
habari jijini Mwanza Mhariri Mkuu wa Baraza la Kiswahili la Taifa bwana Richard
Ntambi amesema watanzania wengi wanaelewana vizuri kwa kutumia lugha ya
Kiswahili hivyo kuwa na sheria zilizo kwenye lugha yao kutasaidia jamii kuzijua
sheria hizo vizuri na kuzifuata tofauti na sasa ambapo zipo kwenye lugha ya
kiingereza ambayo wengi wao hawaifahamu.
“Changamoto kubwa iliyopo hasa
katika masuala ya haki na mahakama ni matumizi ya lugha ya kiingereza hasa kwa
jamii kutoelewa vyema majadiliano yanayofanyika kwenye mahakama hizo na kwenye
hukumu zinazotolewa hali inayopeleka malalamiko mengi na wengine kulazimika
kutumia gharama kupeleka hukumu zao kwa watu kuwasaidia kutafsiri sheria na
hukumu zao hivyo haya yote yatamalizika kupitia kazi hii ya matumzi ya Kiswahili
mahakamani” alisema Bwana Ntambi.
Mhariri Mkuu huyo kutoka BAKITA amesema
wanatambua changamoto ya uwepo wa misamiati michache ya Kiswahili kukidhi ile
ya kiingereza lakini jitihada zinafanyika kuhakikisha kuwa misamiati ya
Kiingereza inapata misamiati sahihi kwa lugha ya Kiswahili kwa kutafuta kutoka
kwenye misamiati ya makabila mbalimbali nchini na pale inapokwama wanatumia
njia ya utohozi wa misamiati hiyo ya kiingereza kwakuwa ni njia pia
inayokubalika.
Kwa upande wake Mwandishi maarufu
wa riwaya na kazi za sanaaa Wakili na Profesa wa Sheria Prof. Abdalah Safari
amesema kazi hiyo kubwa na nzuri inayofanywa na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa
Sheria imekuwa ni kilio cha muda mrefu cha Watanzania wengi na wadau wa Sheria
na Haki.
Mwandishi maarufu wa riwaya na kazi za sanaaa Wakili na Profesa wa Sheria Prof. Abdalah Safari akitoa salamu zake wa wadau hao wa Kiswahili na sheria nchini |
Prof. Safari amesema baada ya
kazi hiyo sasa ni muhimu kuwa na kamusi ya sheria kwa Kiswahili ingawa tayari Ofisi
ya Mwandishi Mkuu wa Sheria imetengeneza Istilahi za Kiswahili ambazo
zinatakiwa pia kupitiwa kwa pamoja na wataalamu wa sheria na lugha ili kujiridhisha na usahihi
wake .
“Pamoja na kutengenezwa kwa
istilahi hizo za kiingereza kwa lugha ya Kiswahili sasa ni wakati wa kufikiria
kitu kikubwa zaidi kama kamusi rasmi ya sheria kwa kiswahili ili kuwezesha hata
zoezi la ufasiri kuwa jepesi na kujenga uelewa wa pamoja kwa kila mtu na kila
mdau wa sheria” alibainisha Prof. Safari.
Prof. Safari alieleza kuwa
Waingereza walitawaliwa na Warumi na kulazimishwa kutumia lugha ya kilatini
kwenye sheria zao lakini baada ya kujikomboa wakagundua mtu anafanya vizuri
jambo kwa lugha mama hivyo wakabadilisha, kwahiyo na Watanzania lugha mama ni
Kiswahili.
“Sheria inasema kutojua sheria
sio utetezi lakini kama mimi siijui sheria na nikavunja maana yake siunanionea?
Hivyo kuwa na sheria za Kiswahili kutaleta haki kwa watu wote maana watakuwa
wanaweza kuzisoma sheria na kuzielewa na kuzifuata” Alifafanua Prof. Safari.
Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria
inaendelea kutekeleza maazimio ya Serikali iliyoyatoa Mwaka 2021 kupitia Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupitisha marekebisho ya Sheria ya Tafsiri
za Sheria ambapo pamoja na mambo mengine iliweka sharti kwamba lugha ya sheria
sasa ni Kiswahili.
MATUKIO KATIKA PICHA NI WATAALAMU WA KISWAHILI NA SHERIA WAKIENDELEA NA KAZI YA KUPITIA MUONGOZO WA UFASILI WA SHERIA.