Na. Edmund Salaho – Udzungwa
Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA) leo Aprili 08, 2025 imeagiza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa kubuni mazao mapya ya Utalii kwa kushirikiana na jamii inayozunguka Hifadhi hiyo.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Mradi wa REGROW ndani na nje ya eneo la Hifadhi hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA Jenerali (Mstaafu) George Waitara alisema,
“Niwapongeze kwa Elimu mnayoitoa kwa jamii kuhusu Uhifadhi na Utalii, tunaenda vizuri nisisitize kubuni mazao mapya ya Utalii kwa kushirikiana na jamii inayozunguka Hifadhi”.
Naye, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini – TANAPA Dkt. Robert Fyumagwa aliipongeza Menejimenti ya Hifadhi hiyo kwa namna ambavyo imewekeza katika kutoa elimu ya Uhifadhi na Utalii kwa wanajamii wanaozunguka Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Massana Mwishawa alisema Shirika kupitia Hifadhi ya Taifa Milima Udzungwa imefanikiwa katika kuhifadhi rasilimali misitu na wanyama wanaopatikana katika Hifadhi hiyo.
“TANAPA kupitia Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa imeshuhudia ongezeko kubwa za watalii pamoja na mapato lakini lengo la kuanzishwa Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa ni kulinda Bioanuai na vyanzo vya maji na hilo lengo tumefanikiwa sana” alisema Mwishawa
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya REGROW katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dora Batiho ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa alieleza kuwa hifadhi inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa miundombinu ya utalii (Canopy Walkway) na kuongeza kwenye jamii zinazozunguka Hifadhi zimenufaika kupitia Benki Hifadhi za Jamii “Community Conservation Bank” (COCOBA) ambapo Jumla ya shillingi millioni 568 ilitolewa kama fedha ya kutekeleza miradi ya vikundi 35 vilivyopo vijiji vya (Mang’ula B, Msufini na Msosa) Vikundi ambavyo vina wanachama 590 huku Miradi iliyochaguliwa na vikundi ikiwa ni pamoja na miradi ya kilimo (mpunga, miwa na nyanya), ufugaji (kuku wa mayai, kuku wa nyama, bata, samaki na nyuki), mapambo, mashine za kusaga, na kukoboa nafaka.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Msufini kilichopo Kilombero Bw. Nicodem Mwalongo alibainisha faida zinazopatikana kupitia mradi wa REGROW na COCOBA ni pamoja na kuboreka kwa Hali ya Uhifadhi wa mazingira, Kuimarika kwa mahusiano kati ya hifadhi na jamii zinazozunguka hifadhi, Kuboresha makazi ya wanachama, Kuongeza mashamba na kulima Kilimo cha Kisasa, pia wanachama wameweza kuanzisha biashara mpya kama maduka na biashara ndogondogo, Mradi wa elimu bora kwa watoto 54 pamoja na uhakika wa bima ya afya kwa wanachama wote wa COCOBA.