Na: Calvin Gwabara – Mwanza
Kukamilika kwa Mwongozo wa Ufasili
wa Sheria, Istilahi za Kisheria pamoja na ufasili wa sheria kuu 446 za Tanzania
kutasaidia jamii kuzielewa, kuzifuata na kupunguza kufanya makosa yanayotokana
na kutojua kwao sheria sambamba na utoaji wa haki.
Hayo yamebainishwa na Mwandishi
Mkuu wa Sheria Bwana Onorius Njole wakati akizindua kikosi kazi maalumu cha
wataalamu wabobevu wa Kiswahili nchini kutoka Chuo Kikuu Huria,Chuo Kikuu cha
Dar es salaana, Chuo Kikuu cha Dodoma ,Baraza la Kiswahili (BAKITA) na
wataalamu wa sheria waliokutanishwa jijini Mwanza kwa lengo la kuhakiki Muongozo
wa Ufasili wa Sheria na Istilahi za Kisheria zilizoandaliwa na Ofisi ya
Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Mwandishi huyo mkuu wa sheria
amesema lengo la Mwongozo huo ni kusaidia kujenga uelewa wa pamoja wa misingi
ya ufasili kwakuwa kuna changamoto ya kutengeneza itungo kwa kutumia misamiati
ya Kiswahili. Alieleza kuwa wamebaini kuwa wakati mwingine kwenye kutafsiri
wanajikuta wanataka kubadili tungo za kiingereza ili zibaki maana ile ile na
hivyo kujikuta haieleweki na haibebi yale masharti ya kisheria yaliyopo katika kifungu
kilichopitishwa na Bunge. Hivyo Mwongozo huu utawezesha kuwa na mfanano wa
tafsiri.
“Tangu nchi yetu ipate uhuru
tumekuwa tukitunga sheria kwa lugha ya kiingereza lakini zaidi ya asilimi 80 ya
watanzania wanatumia lugha ya Kiswahili kama lugha mama, na tunapotaka kila mtu
kufuata sheria maana yake lazima aijue na kuilewa vizuri lakini hawawezi
kuilewa kama ipo kwenye lugha ambayo hawaijui huku tukitaka waifuate, hivyo
ufasili wa sheria utasaidia sana jamii kupunguza kufanya makosa kwa kujua masharti
ya sheria wanayotakiwa kuzingatia haswa kwa kuwa kutojua sheria sio utetezi pale
unapofanya makosa” alisema Bwana Njole.
Aliongeza “Kumekuwa na changamoto
kwamba utekelezaji wa sheria umekuwa ni mdogo,uzingatiaji wa matakwa ya sheria
umekuwa ni mdogo na wakati mwingine sio kwasababu ya ukaidi ila ni kwa sababu
ya lugha inayotumika kwenye sheria, hivyo kwa zoezi hili tunalenga kuwawezesha
wananchi wazijue sheria na kuzizingatia lakini kusaidia utekelezaji wa sheria
hizo na utoaji wa haki”.
Mwandishi huyo mkuu wa sheria
amesema Serikali kwa sasa imeweka msukumo mkubwa kwenye kuhamasisha uwekezaji
nchini lakini kumekuwa na migogoro kwenye maeneo mbalimbali kati ya wawekezaji na
wananchi na ukifuatilia unakuta wananchi hawaifahamu sheria inayosimamia
uwekezaji husika hivyo kuna umuhimu wa pande zote mbili kuelewa wajibu wa kila
upande kama sheria inavyoelekeza.
Hata hivyo Bwana Njole amesema
msukumo huohuo umeelekezwa pia kwenye mahakama za Tanzania kuendesha kesi na
kutoa hukumu kwa lugha ya Kiswahili ambayo ndio lugha inayoeleweka na watu
wengi hivyo mahakama kama chombo cha toa haki lazima ipate sheri kwa lugha ya
Kiswahili ili iweze kuzitafsiri vizuri.
Amesema kuwa kufuatia umuhimu huo
ni lazima sasa zoezi la ufasili wa sheria lifanyike katika misingi ya ufasili
inayofahamika kwa kila mtu na ndio maana wamemua kuandaa Muongozo wa Ufasili
ili hata pale mahakama inapokutana na utata kwenye maeneo fulani ya sheria
iliyofasiliwa wataweza kutumia muongozo huo kujua misingi iliyotumika kufasili
sheria husika yenye utata.
“Pamoja na faida zote hizo lakini
kubwa zaidi ni mahakama kutafsiri sheria na kutoa haki kwa Kiswahili katika
utoaji wa haki na sheria kwa lugha ya Kiswahili pia kutasaidia kukuza
demokrasia,Uchumi, Uwekezaji na maendeleo ya watu kwenye nyanja zote”
alibainisha Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Kwa upande wake mmoja wa wajumbe
wa kikosi kazi hicho ambaye ni mwandishi maarufu wa riwaya na kazi za sanaaa
Wakili na Profesa wa Sheria Prof. Abdalah Safari amepongeza jitihada kubwa
iliyofanyika katika kuhakikisha kunakuwepo na Muongozo wa Ufasili wa Sheria
nchini ili zieleweke kwa maana moja.
Mwandishi maarufu wa riwaya na kazi za sanaaa Wakili na Profesa wa Sheria Prof. Abdalah Safari ambaye ni mmoja wa wajumbe wa kikosi kazi hicho akitoa neno wakati wa uzinduzi. |
“Niipongeze sana Ofisi ya
Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa kazi hii kubwa iliyofanyika maana baada ya
Serikali kutoa tamko la kila sheria kutungwa na kutafsiriwa kwa lugha ya
Kiswahili itapelekea watu wengi kujitokeza kufanya kazi hiyo japo kimsingi
msimamizi mkuu wa jambo hilo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia
Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria” Alieleza Prof. Safari.
Aliongeza “Sasa kufuatia uhitaji
huo na watu watakapojitokeza kufasili sheria lazima kuwepo na Mwongozo maalumu
wa kuufuata kwenye kufanya kazi hiyo ili kuhakikisha watumiaji wa sheria hizo
wanapata maana moja na sio maana tofauti na kuleta mgongano kwenye kutoa haki
mahakamani”.
Mdau huyo maarufu wa Kiswahili
nchini amesema baada ya zoezi hilo sasa ni muhimu kuwepo kwa kamusi ya sheria
na maneno yake kwa lugha ya Kiswahili ili kuweza kutafsiri yale maneno ya
kiingereza yanayotumika kwenye sheria na dhana zake kwa Kiswahili fasaha.
Nae Mwandishi Mkuu wa Sheria
Mstaafu, Bi Sarah Barahomoka ambaye ndiye mwenyekiti wa kikosi kazi hicho
amesema kazi hiyo wanayoifanya inaingia kwenye historia kwa kuanda muongozo wa
ufasili wa sheria nchini kwakuwa sheria zimekuwa zikifasiliwa kwa utashi wa mtu
na sio kwa kufuata muongozo hivyo kazi hiyo wameahidi kuifanya kwa weledi
mkubwa ili isaidie kuweka misingi ya ufasili wa sheria na katika utoaji wa haki
na uelewa wa sheria kwa kila mtu.
Itakumbukwa kuwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wakati akihutubia Bunge alisisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa wa sheria kwa wananchi kwa kutunga sheria kwa lugha ya Kiswahili. Katika kutekeleza azma hiyo, Mwaka 2021 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Tafsiri za Sheria ambapo pamoja na mambo mengine iliweka sharti la kwamba lugha ya sheria sasa ni Kiswahili na lugha ya kutumika katika vyombo vya utoaji haki nchini nay oni Kiswahili
Mwandishi Mkuu wa Sheria Mstaafu, Bi Sarah Barahomoka ambaye ndiye mwenyekiti wa kikosi kazi hicho akitoa neno kabla ya kumkaribisha Mwandishi Mkuu wa Sheria kuzungumza na wajumbe hao. |
.
Wajumbe wa Kikosi kazi hicho pamoja na sekretarieti yao kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mgeni Rasmi Bwana Onorius Njole. |