Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo April 8, 2025
.jpeg)
Mwenge wa Uhuru umezindua mradi wa boti ya doria na ukaguzi baharini katika soko la samaki, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, utakaodhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na uvuvi, kuzuia uvuvi haramu na biashara za magendo zinazofanyika baharini.
Aidha, mradi huu ambao umegharimu milioni 40.603 pia utaimarisha usimamizi wa raslimali za uvuvi.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, ameridhishwa kuzindua mradi huo.
Vilevile, Mwenge wa Uhuru ulizindua mradi wa ununuzi wa gari na vifaa vya uzoaji taka kwa kikundi cha vijana cha SAFISHA Mazingira, kata ya Nianjema, ulio gharimu milioni 150.600.
Mradi mwingine uliozinduliwa ni upanuzi wa tanki la maji Kidomole, ambao ulianzishwa kwa kuwekwa jiwe la msingi mwaka 2024, na wenye thamani ya milioni 334.240.
Mradi huu ulianza mwaka wa fedha 2023/2024 na umetekelezwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa manunuzi (NeST).
Pamoja na hayo, mradi wa ujenzi wa boksi na kalvati barabara ya Kimalang’ombe – Makofia lenye thamani ya milioni 121.951 kutoka kwa serikali kupitia TARURA, pia uliwekwa jiwe la msingi.
Akipokea Mwenge wa Uhuru tarehe 8 Aprili 2025 kutoka Wilaya ya Mafia, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, alieleza kuwa miradi sita imepitiwa, kati ya hiyo mmoja umewekwa jiwe la msingi na mingine kuzinduliwa, na jumla ya gharama za miradi hii ni milioni 747.5.
Akikabidhi Mwenge huo, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, alisema kuwa mwenge wa Uhuru ukiwa Wilaya ya Mafia, miradi 15 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.8 imefanyika.
“Kati ya miradi hiyo, 11 imekaguliwa, 3 imezinduliwa, na 1 umewekewa jiwe la msingi, kwa umbali wa kilomita 64.9,” alifafanua Aziza.