Na Mwandishi Wetu, Kiteto
MRADI wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), umekabidhi cheti cha haki ya kimila ya umiliki ya ardhi ya kimila ya umiliki wa ardhi yam situ mtakatifu kwa jamii ya Akie iliyopo Kiteto mkoani Manyara ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya mradi huo iliyotolewa Mwaka 2022.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hati hiyo iliyoambatana na uzinduzi wa zahanati sambamba na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa jamii hiyo, katika kitongojii cha Napilikunya, Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara, Meneja Mkuu wa EACOP Tawi la Tanzania, Bi Wendy Brown amesema kuwa hayo ni matokeo ya ushirikiano uliopo kati ya mradi na jamii hiyo.
“Nakumbuka nilikuja hapa mwezi wa Julai mwaka 2022, wakati wa hafla ya utiliaji saini randama ya ridhaa huru ya uelewa kabla ya utekelezaji wa mradi (FPIC) ambapo mlitoa ombi maalum kwamba mnaomba ardhi yenu ya matambiko ilindwe kisheria na tulihaidi kulishughulikia, imepita miaka mitatu sasa ambapo leo tumerudi kutimiza ahadi yetu,” alisema Bi Brown.
Alisema tukio hilo ni ushahidi tosha wa namna ambayo EACOP imejipambanua kulinda na kusimamia mazingira, tamaduni pamoja na maendeleo endelevu ya jamii za pembezoni.
“EACOP inaamini maendeleo sio miundombinu pekee bali ni pamoja na mila na desturi sambamba na maisha bora, kwa kulitambua hilo, leo tutakabidhi hati ya hakimiliki ya kimila kwa familia saba ambazo ziliguswa na mradi, alisema Bi. Brown.
Aidha, Bi Brown alisema katika wilaya ya Kiteto pekee wamewezesha upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa 875 na kati ya hivyo, vyeti 125 ni vya jamii ya Akie, mpaka kufikia sasa vyeti 112 vipo tayari na baadhi vitakabidhiwa kwa watoto wa jamii hiyo.
Bi Brown alisisitiza umuhimu wa tukio hili akisema, “Makabidhiano haya yanawakilisha hatua kubwa katika dhamira yetu ya maendeleo endelevu na uwajibikaji wa kijamii. Kwa kuhakikisha umiliki wa ardhi kwa Msitu Mtakatifu wa Akie na kusaidia kaya zilizoathirika na mradi, tunathibitisha kujitolea kwetu kuheshimu urithi wa kitamaduni na kuhakikisha athari chanya kwa jamii.”
Kwa upande wa Meneja wa ardhi na masuala ya kijamii Tanzania, Jean Lennock aliongeza, “Katika EACOP, tunaelewa umuhimu wa usalama wa ardhi, uhifadhi wa tamaduni, na ustawi wa kijamii. Jitihada hizi ni ushahidi wa ushirikiano wetu endelevu na jamii za wenyeji ili kuleta manufaa ya muda mrefu. Tunajivunia kuwa sehemu ya safari hii na kushuhudia mabadiliko chanya ambayo mradi unaleta katika maisha ya watu.”
Wakati huo huo Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Katibu Tawala, Bi. Mufandii Msaghaa, amesema toka mradi uanze kutekelezwa, walengwa waliopitiwa na mradi huu, mbali ya kunufaika na fidia, wamekuwa wakipewa kipaumbele cha ajira hasa zile za ujuzi wa kati na ujuzi wa chini ili kujikwamua kiuchumi.
“Napilikunya ni miongoni mwa kitongoji ambacho kimenufaika na mradi, ambapo mbali ya kulipwa fidia zahanati pia ilijengwa alisema Bi. Msaghaa.
Bi. Msaghaa alitoa rai kwa wakazi wa kiteto kueshimu maeneo waliyokabidhiwa jamii ya Akie kwani maeneo hayo si sehemu tu ya makazi bali ni maeneo wanayotumia kuabudu sambamba na kutunza kumbukumbu za tamaduni zao kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Jamii kutoka EACOP, Bi. Fatuma Msummi amesema mradi umekuwa ukifanya kazi kwa karibu na Serikali, (NGOS) na viongozi wa kimila katika kuhakikisha jamii za pembezoni na zilizoguswa na mradi zinanufaika.
“Hatua hizi za EACOP ni utekelezaji wa sheria na taratibu za kimataifa ambazo zinaitaka EACOP kuheshimu mila na tamaduni za watu wa asili wakati wa utekelezaji wa mradi, alisema Bi. Msummi.
Naye Mshauri wa EACOP kuhusu vigezo vya kimataifa kwa jamii za pembezoni, Dkt. Elifuraha Laltaika amesema EACOP imekuwa ikifanya kazi kwa uwazi na kujitoa katika kuwajengea uwezo jamii.
Toka mradi uanze kutekelezwa, walengwa waliopitiwa na mradi huu, mbali ya kunufaika na fidia, wamekuwa wakipewa kipaumbele cha ajira hasa zile za ujuzi wa kati na ujuzi wa chini ili waweze kuchangia kukuza pato la taifa, alisema.
Bw Yohana Lemama ambaye ni Mwenyekiti wa Jamii ya Akie, mbali ya kuipongeza EACOP kwa kueshimu tamaduni na kuthamini mila na desturi zao, amesema uwepo wa hati miliki ya ardhi utawasaidia kutunza mila na utamaduni zao kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Uwepo wa EACOP umetuwezesha sisi jamii za pembezoni kujengewa uwezo kwa kupewa mafunzo mbalimbali ikiwemo kupanda mazao kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo, amesema. na kuongeza kuwa uwepo wa mradi umewezesha ujenzi wa barabara, zahanati, shule na ununuzi wa madawati ya kisasa.
Wanahisa wa EACOP ni TotalEnergies yenye asilimia (62), Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) yakimiliki asilimia 15 kila moja na kampuni ya mafuta ya Kichina (CNOOC) ikiwa na asilimia nane.Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto, Bi. Mufandii Msaghaa (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na familia saba ambazo zimeguswa na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) na kukabidhiwa hati ya hakimiliki ya kimila wakati wa hafla ya makabidhiano ya hati miliki ya ardhi ya Kimila ya jamii ya Akie iliyofanyika katika kitongoki cha Napilikunya, Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara. Kushoto kwake ni Bi. Fatuma Msummi, Mkuu wa Kitengo cha Jamii kutoka EACOP. Na watatu kulia ni Meneja Mkuu wa EACOP upande wa Tanzania, Bi. Wendy Brown
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto, Bi. Mufandii Msaghaa (kushoto) na (kulia) ni Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Bw. Edward Ole Lekaita wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa zahanati iliyoghalimu zaidi ya shilingi milioni 102 ikiwa ni fidia za Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) wakati wa hafla ya makabidhiano ya hati miliki ya ardhi ya Kimila ya jamii ya Akie iliyofanyika katika kitongoki cha Napilikunya, Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara. Watatu kulia ni Meneja Mkuu wa EACOP upande wa Tanzania, Bi. Wendy Brown na watatu kushoto ni Meneja Idara ya Ardhi na Ushirikishwaji Jamii kutoka EACOP, Bi. Jean Lennock.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto, Bi. Mufandii Msaghaa (katikati) akizungumza na jamii ya Akie (hawapo pichani) wakati wa hafla ya makabidhiano ya hati miliki ya ardhi ya Kimila ya jamii hiyo iliyofanyika katika kitongoki cha Napilikunya, Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara. Kulia kwake ni kwake ni Meneja Mkuu wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) upande wa Tanzania, Bi. Wendy Brown, kushoto kwake ni Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Vicent Gyunda na kulia ni Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Bw. Edward Ole Lekaita, wapili kulia ni Bi. Jean Lennock, Meneja Idara ya Ardhi na Ushirikishwaji Jamii kutoka EACOP.