Katibu Tawala Mkoa Wa Tabora Dkt John Mboya akizungumza na Maafisa Ununuzi kutoka Mikoa 12 nchini inayofanyika mkoa wa Tabora.
Hao ni Maafisa Ununuzi kutoka Mikoa 12 nchini wakimsikiliza mtoa mada.
Meneja wa Kanda ya Kati na Magharibi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Mhandisi Suma Atupele amesisitiza mafunzo yamelenga kuwajengea uwezo Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi kutoka taasisi za umma.
Na Lucas Raphael,Tabora
SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwajengea uelewa mpana wa matumizi sahihi ya mfumo mpya wa ununuzi wa umma (NeST) Wataalamu wa Ununuzi wa taasisi za umma nchini.
Akifungua mafunzo ya siku 5 kwa Maafisa Ununuzi kutoka Mikoa 12 nchini yaliyofanyika jana Mkoani Tabora, Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt John Mboya ameeleza kuwa mfumo huo ni muhimu sana kwa kuwa unaokoa fedha za serikali.
Alisisitiza kuwa serikali imeamua kutunga upya sheria ya ununuzi wa umma namba10 ya mwaka 2023 pamoja na kanuni zake za mwaka 2024 ili kuboresha sekta hii kwa maslahi mapana ya taifa.
Aidha sheria hii imechochea kuanzishwa na kuanza kutumika kwa Mfumo mpya wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) ambapo taasisi zote sasa zinatakiwa kuanza kutumia mfumo huu ili kuongeza uwazi na ushindani wa zabuni
‘Mfumo wa NeST ni hatua muhimu sana ya matumizi bora ya teknolojia katika sekta za umma, mfumo huu sio tu suluhisho la mchakato wa ununuzi wa umma pia unaongeza uwazi, ufanisi na usimamizi thabiti za rasilimali za umma’, alisema Dkt Mboya.
Dkt Mboya alitoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo zaidi ya 120 kutumia vizuri elimu watakayopewa na kufanya kazi zao kwa weledi na uadilifu mkubwa ili kuleta tija kwa taasisi zao, serikali na jamii kwa ujumla.
Meneja wa Kanda ya Kati na Magharibi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Mhandisi Suma Atupele alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi kutoka taasisi za umma.
Alibainisha kuwa mfumo wa NeST unatoa fursa kubwa kwa wazabuni mbalimbali ikiwa ni pamoja na wazabuni wadogo na wakubwa, makundi maalumu, vijana na wanawake kuhusika kikamilifu katika mchakato wa ununuzi wa umma.
‘Ununuzi wa Umma haujumuishi tu makampuni makubwa, bali pia unaongeza fursa za kiuchumi kwa wadau wadogo na wa kati katika jamii, hivyo wananchi nao wanapaswa kuufahamu vizuri mfumo huu ili kunufaika nao’, alisema Mhandisi Suma .
Aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa chachu ya mabadiliko kwenye michakato ya ununuzi wa umma na kuhakikisha changamoto za ununuzi zinatatuliwa na kupatiwa ufumbuzi ndani ya taasisi zao.