Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewasihi Mabalozi kuwaunganisha Watanzania wanaoishi katika nchi wanazowakilisha (Diaspora) ili waweze kuchangia maendeleo ya Taifa kupitia uwekezaji mbalimbali.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Sweden Mheshimiwa Balozi. Mobhare Matinyi pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji Mheshimiwa Balozi. Hamad Khamis Hamad, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 09 Aprili 2025.
Amesema ni muhimu kuwatambua Watanzania hao kutokana na utaalamu, elimu au ufanyaji biashara na kuwahimiza kuwekeza nchini pamoja na kusikiliza maoni na changamoto zao ili kuzifanyia kazi. Amewataka Mabalozi kuwahimiza Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania kufuata sheria na taratibu za Mataifa husika pamoja na kufanya uwekezaji katika ngazi ya familia zao zilizopo nchini ikiwemo kuwasaidia ndugu zao kupata elimu pamoja na ujenzi wa majengo ya makazi na biashara.
Pia Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuliwakilisha Taifa kwenye nchi hizo. Amewaasa Mabalozi hao kuendeleza ushirikiano wa Tanzania na Mataifa hayo ambao umekuwepo kwa muda mrefu.
Makamu wa Rais amewasisitiza Mabalozi hao kuhakikisha wanakuwa na taarifa za msingi juu ya maendeleo ya Taifa la Tanzania ili kuwa na uwakilishi mzuri katika maeneo yao hususani katika kutekeleza diplomasia ya uchumi. Aidha amewahimiza kuhakikisha wanatambua fursa zinazopatikana nchini ikiwemo rasilimali iki kuweza kuvutia wawekezaji kutoka katika mataifa wanayokwenda kuwakilisha.
Halikadhalika amewasihi kufahamu takwimu za msingi za Mataifa wanayokwenda kuiwakilisha Tanzania ikiwemo fursa mbalimbali, maeneo muhimu ya ukuzaji wa uchumi pamoja na sekta mbalimbali za mataifa hayo. Amesema ni muhimu kuhakikisha wanakuwa na ushirikiano na watunga sera na viongozi wakuu wa sekta binafsi katika mataifa hayo.
Amewaasa kufahamu vema vipaumbele vya Taifa, mikakati mbalimbali pamoja na utekelezaji wake ikiwemo Dira ya Taifa, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na mipango ya maendeleo ya miaka mitano na mwaka mmoja mmoja.
Pia amesema ni muhimu kuendelea kuitangaza lugha ya Kiswahili katika nchi hizo ikiwemo kutafuta fursa ya ajira kwa walimu wa kufundisha lugha hiyo pamoja na ukalimani. Amewahimiza kukuza biashara ya Tanzania na Mataifa hayo ikiwemo kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania pamoja na kuwaunganisha watanzania na fursa mbalimbali za kibiashara.
Makamu wa Rais amesema kwa Mataifa yaliyoendelea kiteknolojia, ni vema kuhakikisha Tanzania inashirikiana nayo ili kuweza kupata manufaa zaidi katika matumizi ya teknolojia kwenye sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na viwanda. Pia amewahimiza Mabalozi kutafuta fursa za mafunzo kwa vijana na kusisitiza zaidi katika ushirikiano wa elimu ya ufundi, utafiti na kujenga uwezo wa kimfumo.
Amewataka kutangaza vema Taifa ili kuvutia zaidi watalii, kushirikiana katika masuala ya mazingira ikiwemo udhibiti wa taka pamoja na kuvutia uwekezaji katika sekta ya afya hususani ujenzi wa viwanda vya dawa.