Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akieleza kuhusu masuala ya ukuaji wa uchumi wakati wa mazungumzo na Balozi wa Tanzania katika nchi ya Ujerumani, anaesimamia pia Poland, Mhe. Hassani Iddi Mwamweta (kushoto), yaliyofaniyika jijini Warsaw Poland, wakati wa ziara ya kikazi nchini humo.
Na. Peter Haule, Warsaw, Poland.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amesema kuwa Serikali inaweka nguvu katika masuala ya ujenzi wa miundombinu hususani ya Reli ya Kisasa (SGR) ili kuchochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji.
Hayo aliyasema jijini Warsaw Poland wakati wa mkutano wake na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani ambaye pia anasimamia nchi ya Poland, Mhe. Hassani Iddi Mwamweta, wakati wa ziara yake ya kikazi nchini humo.
Dkt. Nchemba alisema kuwa vipande viwili vya Reli ya Kisasa vya Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Dodoma vimekamilika na kuanza kufanya kazi ambapo kipande cha tatu na nne kutoka Makutopora hadi Tabora na Tabora hadi Isaka ndilo eneo ambalo zinatafutwa fedha ili kukamilisha ujenzi wake.
Aidha, Dkt. Nchemba alimpongeza Mhe. Balozi Mwamweta kwa kusimamia vizuri diplomasia ya uchumi katika nchi anazoiwakilisha Tanzania na kusisitiza kuwa Tanzania ina maeneo mengi yanayofaa kwa uwekezaji na kumtaka aendelee kuhimiza uwekezaji ambao utachangia kukuza uchumi wa nchi.
Alisema kuwa miundombinu mingine iliyopewa kipaumbele ni pamoja na nishati, na miundombinu ya uzalishaji ya kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili ambayo ina lengo la kutengeneza kesho iliyobora zaidi na kusisitiza umuhimu wa vijana kupatiwa ujuzi wa kuzalisha pamoja na kutafuta masoko.
Kwa upande wake Mhe. Balozi Mwamweta, akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu yake, alieleza kuwa jitihada zinazofanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha miundombinu ya Reli zinaonekana na wadau wa maendeleo, jambo ambalo linarahisisha kazi yake ya kuinadi nchi katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.
Alisema kuwa nchi nyingi zilizoendelea katika Bara la Ulaya ziliwekeza kwenye miundombinu wezeshi kama Reli na kuweza kuchochea kwa kasi maendeleo yao jambo ambalo Tanzania pia imekuwa na mwelekeo huo ambao matokeo yake yanaonekana kwenye duru za kimataifa.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akieleza kuhusu masuala ya ukuaji wa uchumi wakati wa mazungumzo na Balozi wa Tanzania katika nchi ya Ujerumani, anaesimamia pia Poland, Mhe. Hassani Iddi Mwamweta (kushoto), yaliyofaniyika jijini Warsaw Poland, wakati wa ziara ya kikazi nchini humo.

Balozi wa Tanzania katika nchi ya Ujerumani, anaesimamia pia Poland, Mhe. Hassani Iddi Mwamweta (kushoto), akieleza mtazamo wa wadau wa maendeleo kuhusu jitihada za kukuza Uchumi nchini katika mkutano na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati wa ziara ya kikazi jijini Warsaw Poland.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiongoza Mkutano kati yake na Balozi wa Tanzania katika nchi ya Ujerumani, anaesimamia pia Poland, Mhe. Hassani Iddi Mwamweta (kushoto), jijini Warsaw Poland, akiwa katika ziara ya kikazi nchini humo.

Baadhi ya Wajumbe kutoka Wizara ya Fedha na Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani, wakifuatilia Mkutano kati ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Balozi wa Tanzania katika nchi ya Ujerumani, anaesimamia pia nchi ya Poland, Mhe. Hassani Iddi Mwamweta, uliofanyika jijini Warsaw Poland, katika ziara ya kikazi nchini humo.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Warsaw Poland)