“Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme katika Bwawa la Julius Nyerere kwa gharama ya shilingi trilioni 6.6. Ujenzi wa mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 2,115 kwa siku umekamilika. Hadi Machi 2025, jumla ya megawati 2,115 zimeunganishwa kwenye gridi ya taifa na hivyo kuongeza kiwango cha umeme katika gridi ya taifa kufikia megawati 4,031.7. Kuanza kwa uzalishaji wa umeme katika mradi huo kumeongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuwa chachu ya kasi ya maendeleo ya nchi.
Katika kipindi cha Novemba, 2020 hadi Februari, 2025, Serikali pia imeunganisha umeme katika vijiji 4,071 kwa gharama ya shilingi bilioni 1,593 na hivyo kuwezesha vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara kuunganishwa na umeme.
Hatua inayofuata baada ya kukamilisha mradi wa kupeleka umeme katika vijiji vyote, ni kupeleka umeme kwenye vitongoji ambapo jumla ya vitongoji 33,657 kati ya 64,359, sawa na asilimia 52.3 vimeunganishwa na huduma ya umeme. Usambazaji wa umeme katika vijiji na vitongoji utawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hususan zinazohitaji nishati ya umeme zikiwemo kuchomelea vyuma, useremala, kuchakata nafaka na kuchenjua madini.” Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akisoma Hotuba ya Bajeti ya Ofisi yake na Bunge 2025/26