Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Kusogezwa kwa huduma ya upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani itaondoa kero ya wananchi ya kusafiri umbali wa kilomita 40 kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi.
Akizungumza kabla ya kuzinduliwa kwa mradi huo,wakati wa mbio za mwenge wa Uhuru halmashauri ya wilaya ya Kibaha, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Christopher Ngendello, alisema hospitali hiyo ilipokea sh. milioni 300 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya upasuaji.
Dkt. Ngendello alifafanua, vifaa vilivyonunuliwa ni pamoja na mashine ya usingizi, vitanda 30, mashine ya kemia, magodoro 30, makabati ya dawa, jokofu za kuhifadhia damu na viti vya kuchangia damu.
Alieleza ,huduma hiyo ilianza kutolewa mwezi Machi mwaka huu na hadi kufikia tarehe 8 Aprili, wagonjwa 16 walikuwa wamepata huduma hiyo.
Kwa mujibu wa dkt Ngendello ,kutolewa kwa huduma hiyo pia kupunguza gharama za sh. milioni 24 hadi 30 ambazo zilikuwa zinatumika kwa ununuzi wa mafuta na matengenezo ya magari ya kubebea wagonjwa.
Akizindua mradi huo, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ussi, aliwataka wananchi kutumia huduma zinazotolewa katika hospital hiyo badala ya kuendelea kusafiri umbali mrefu.
Vilevile aliwahimiza wananchi kupambana na magonjwa ya malaria na UKIMWI na madawa ya kulevya kwa kuzingatia elimu inayotolewa na wataalamu wa afya ili kutokomeza magonjwa hayo.
Miongoni mwa miradi iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru ni ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja katika Shule ya Msingi Uhuru, mradi wa vijana wa ufugaji kuku, sanjali na ukaguzi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Amali iliyoko katika Kijiji cha Minazimikinda.