Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga amewataka wachimbaji na wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite kuiga mambo mazuri yaliyofanywa na Mkurugenzi wa kampuni ya Chusa Mining LTD, Joseph Mwakipesile katika kusaidia miradi ya jamii.
RC Sendiga ameyasema hayo mara baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa wodi ya wanawake, watoto na ofisi ya madaktari wa kituo cha afya Mirerani inayojengwa kwa msaada wa kampuni ya Chusa Mining LTD kwa gharama ya shilingi milioni 120.
RC Sendiga amesema wachimbaji wengine wangeiga mambo mazuri yanayofanywa na kampuni ya Chusa Mining LTD kwa kufanikisha miradi ya maendeleo kwa jamii ya Mirerani wangepiga hatua zaidi.
“Tunaipongeza kampuni ya Chusa Mining LTD kwa kujenga majengo haya yatakayogharimu shilingi milioni 120, tunawasihi wadau wengine wa madini kuiga mambo mazuri kama haya kwa kusaidiana na Serikali kufanikisha miradi ya jamii,” amesema RC Sendiga.
Hata hivyo, RC Sendiga amempongeza mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mirerani, Dkt Namnyaki Lukumay kwa namna anavyosimamia ujenzi wa majengo ya idara ya afya kwa uzalendo mkubwa.
“Huyu daktari ni mwanamama shupavu tumeona kituo cha afya cha Tanzanite kata ya Mirerani amesimamia vyema na sasa ujenzi wa jengo la mionzi katika kituo cha afya Mirerani kata ya Endiamtu anasimamia vizuri,” amesema RC Sendiga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga ameipongeza kampuni ya Chusa Mining LTD, kwa kujenga majengo hayo ya wodi ya wanawake na watoto katika kituo cha afya Mirerani.
“Tumeona CSR kwa vitendo kupitia Chusa Mining LTD, ila tunaomba mfuate muongozo wa majengo ya serikali katika idara ya afya ikiwemo ramani yake na rangi ili zifanane,” amesema Kanunga.
Meneja wa kampuni ya Chusa Mining LTD, Thadey Joseph ameishukuru Serikali kwa kuwapa ushirikiano katika ujenzi wa majengo hayo ya wodi ya wanawake, watoto na ofisi za madaktari.
“Tunatarajia majengo haya yatakamilika kwa wakati na kisha tutawakabidhi funguo na kisha jamii ianze kupata huduma tarajiwa,” amesema.

