Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limepokea rasmi boti ya kisasa ya ‘ambulance’ kwa ajili ya shughuli za utafutaji na uokoaji (Search and Rescue – SAR), hatua inayolenga kuboresha usalama wa majini katika Maziwa Makuu hususan Ziwa Victoria.
Akizungumza katika hafla ya kupokea boti hiyo, leo tarehe 11 Aprili 2025 katika Bandari ya Mtwara, Kaimu Meneja wa Usajili na Ukaguzi wa Meli kutoka TASAC, Mha. Said Kaheneko, amesema kuwa ununuzi wa boti hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 ambapo kupitia TASAC, Serikali imepanga kununua jumla ya boti tano za utafutaji na uokoaji.
Boti hiyo ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 16 kwa wakati mmoja na ina vitanda vinne (4) vya wagonjwa, wakiwemo wawili (2) wanaohitaji uangalizi maalum (ICU), na sehemu ya chini inayoweza kubeba wagonjwa 12 pamoja na huduma ya kwanza kwa wagonjwa zinaweza kutolewa ndani ya boti hiyo kabla ya kuwafikisha hospitalini, jambo litakaloongeza uwezekano wa kuokoa maisha.
Aidha, Mha. Kaheneko amesema boti nyingine mbili (2) za SAR ambazo ni sehemu ya Mradi wa Kikanda wa Usafiri na Mawasiliano wa Ziwa Victoria (MLVMCT) zipo katika hatua ya mwisho ya ukaguzi na zinatarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwezi Mei. Ameongeza kuwa mnamo tarehe 3 Aprili 2025, TASAC ilisaini mkataba mwingine wa manunuzi ya boti mbili zaidi, ambazo zitakamilika ifikapo Septemba 2025 na kwa mwaka wa fedha 2025/2026, tayari bajeti imetengwa kwa ajili ya ununuzi wa boti tatu (3) zaidi na kufanya TASAC kuwa na jumla ya boti saba (7) za SAR.
Nae Meneja Uhusiano na Masoko wa TASAC, Bw. Saidi Mkabakuli amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mradi huu na kusema kuwa boti hii ni faraja kubwa kwa wakazi wa visiwani na wale wanaofanya shughuli zao kwenye Ziwa Victoria.
“Tunamshukuru Mhe. Rais kwa kuwezesha upatikanaji wa boti ambayo inapeleka faraja kwa wakazi wa maeneo ya Ziwa Victoria hasa wanaojishughulisha shughuli za kiuchumi ziwani au wanaoishi kwenye visiwa, ambulance boat hii ni msaada mkubwa wakati wa dharura majini,” amesema Bw. Mkabakuli.
Ameongeza kuwa kupatikana kwa boti hii kutaimarisha usalama majini, kuokoa maisha, na kusaidia shughuli za kiuchumi zinazotegemea maziwa makuu ya Tanzania.