Na Silivia Amandius,
Kagera,
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Damas Ndumbaro, anatarajiwa kuzindua rasmi Kampeni ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria (MSLAC) tarehe 14 Aprili, katika mkoa wa Kagera. Kampeni hiyo itadumu kwa siku tisa na inalenga kutoa msaada wa kisheria bila malipo kwa wananchi wote, hususan wale wasioweza kugharamia huduma za kisheria.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, Mkurugenzi wa Kampeni hiyo, Bi. Ester Msambazi, alisema kuwa huduma hiyo inalenga kuwanufaisha wananchi wenye changamoto mbalimbali za kisheria, ikiwemo migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa na masuala ya jinai.
“Tumeshafikia mikoa 23 na sasa tupo katika mkoa wa 24, Tanga. Kwa sasa tumewasili Kagera ambapo tutatoa huduma katika wilaya zote, tukilenga kata 10 na vijiji 30 kila siku. Lengo ni kuwafikia takribani asilimia 75 ya wananchi wote wenye matatizo ya kisheria,” alisema Bi. Msambazi.
Huduma zitakazotolewa zitajumuisha ushauri wa kisheria, uwakilishi mahakamani kwa waliokosa uwezo wa kuwalipa mawakili, pamoja na uandikishaji wa vitambulisho vya taifa na vyeti vya kuzaliwa. Mamlaka zote zinazohusika na masuala ya sheria zitashiriki katika kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi ndani ya siku hizo tisa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, aliwataka wananchi wote kujitokeza kwa wingi kufikisha migogoro yao, hasa ya ardhi, ambayo ni changamoto kubwa katika mkoa huo.
“Tunataka kuona wananchi wanapata suluhu ya changamoto zao. Kupitia kampeni hii, wataalamu wajifunze mbinu mpya na wataendeleza huduma hata baada ya kampeni. Nimeagiza wakuu wa wilaya na wataalamu kuendelea kusikiliza kero za wananchi kila Jumanne na Alhamisi,” alisema Mwassa.
Aliongeza kuwa anatarajia kampeni hiyo itasaidia kuongeza furaha na utulivu miongoni mwa wananchi kwa kuwa kesi nyingi zitakuwa zimetatuliwa.