NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewaonya wananchi na watumiaji wa usafiri wa majini kuwa waangalifu kutokana na hali mbaya ya hewa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Meneja wa TMA Kanda ya Ziwa, Agustine Nduganda, amesema leo kuwa, tathmini ya mvua za masika zinazoendelea kunyesha inaonesha kuwa katika Wilaya ya Ilemela, mvua zitakuwa za wastani au chini ya wastani, zikiwa kati ya milimita 350 hadi 400 kwa kipindi cha Januari hadi Mei, 2025.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa mamlaka husika pamoja na wananchi kuchukua tahadhari stahiki ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, hasa kwa wasafiri wa majini.
“Takwimu za TMA za Machi 7 mwaka huu zinaonesha uwepo wa mvua kubwa, ambapo Machi 9 kulinyesha mvua nyingi jijini Mwanza. Aidha, tunatarajia ongezeko la vipindi vya mvua kubwa katika mwezi wa Aprili, hasa hadi wiki ya tatu ya mwezi huo, yaani Aprili 21, 2025,” amesema Nduganda.
Ameeleza kuwa mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo yote ya Mwanza na Ziwa Victoria zimeongezeka kwa kiwango kikubwa, hivyo ni muhimu wananchi wachukue tahadhari kwa kusafisha mifereji ili kuepuka mafuriko, huku wakulima wakitakiwa kuendelea na palizi pamoja na kunyunyizia dawa ili kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao.
“Tunaendelea kufuatilia mwenendo wa mvua na kutoa tahadhari kwa wakati. Kwa mfano, Aprili 9 mvua kubwa ilinyesha na kusababisha daraja la Mkuyuni kufurika maji. Tunawajulisha wavuvi na wasafirishaji wa majini kuhusu hali ya hewa kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu kupitia vikundi vya BMU, saa 9 alasiri kwa wanaoelekea ziwani jioni na saa 9 alfajiri kwa wanaoingia majini asubuhi,” amefafanua.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Buswelu (CCM), Sarah Ng’hwani, amewataka wakazi wa kata hiyo kufuata maelekezo ya TMA, akibainisha kuwa kata hiyo ina eneo la bonde la kilimo na mwinuko, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa athari endapo tahadhari haitachukuliwa mapema.
Hata hivyo, licha ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kunyesha usiku wa kuamkia leo, TMA Kanda ya Ziwa imethibitisha kuwa hakuna madhara makubwa yaliyoripotiwa kufuatia mvua hizo.ss