Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga akizungumza na baadhi ya wadau wa lishe mkoani Rukwa.
……………….
Na Neema Mtuka Sumbawanga,
Rukwa, Ili Jamii iweze kustawi katika masuala mtambuka, wadau wa lishe katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wametakiwa kuifanya ajenda ya lishe kuwa ya kudumu katika ngazi zote za Jamii.
Akizungumza leo Aprili 12, 2025 katika kikao cha Kamati Jumuishi ya Lishe kwa Robo ya Tatu (Januari – Machi) mwaka wa fedha 2024/2025, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Nassir Kirusha amesisitiza kuwa suala la lishe linamhusu kila mmoja, baba, mama, watoto, makundi maalumu na Jamii yote.
Kirusha amehimiza elimu ya lishe kuendelea kutolewa katika mikusanyiko rasmi na isiyo rasmi vikiwemo vijiwe vya mazungumzo, maeneo ya shughuli za kijamii na katika taasisi za Serikali.
Aidha, ametoa pongezi kwa Kamati ya Lishe kwa kazi kubwa ya kuendelea kuelimisha jamii na kuhakikisha watu wanapata uelewa sahihi na wa kina kuhusu lishe bora.
“Ni muhimu kuhakikisha tunaifikia jamii kwa kutoa elimu ya lishe itakayowasaidia kuepukana na magonjwa yatokanayo na ukosefu wa lishe bora “amesema Kirusha
Nao baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Sumbawanga akiwemo Annacreta Michese amesema elimu ya lishe inahitajika kwani wengi wao wamezoea aina Moja ya chakula.
“Unakuta mama anawapikia watoto chakula cha wanga peke yake bila kuchanganya na makundi mengine ya chakula jambo ambalo linadhoofisha ustawi wa afya kwa Jamii”amesema Michese
Kwa upande wake afisa lishe manispaa ya Sumbawanga Wittiness Williams amesema watoto,mama wajawazito na vijana balehe wanahitaji kupata makundi yote ya vya kula.
Afisa huyo ametaja makundi ya vyakula kuwa ni vyakula vya wanga,vyakula vya mafuta ,vyakula vya protini,vitamini,vyakula vya mizizi.
Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kupitia Viongozi wa Serikali, wataalamu wa lishe, kamati ya lishe, idara mtambuka na wadau mbalimbali wanaendelea kuwafikia wananchi kwa nyakati tofauti ili kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu umuhimu wa lishe bora.
Kwa pamoja, wadau hao wamedhamiria kuendelea kutoa elimu ya lishe bora kwa Jamii huku wakihimiza umuhimu wa mlo kamili nyumbani na shuleni, kwa ajili ya afya na ustawi wa Jamii kwa ujumla.