Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa (Mb), amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), inajenga minara 38 kwa ruzuku ya shilingi bilioni 7.1 Mkoani Kilimanjaro, ikiwemo minara 6 inayojengwa katika wilaya ya Mwanga kwa lengo la kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za mawasiliano ya uhakika.
Waziri Silaa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi katika kijiji cha Karamba Ndea wakati wa ziara ya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro, hususani katika lango la kuingia na kutoka watalii la Ndea kwenye hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.
Mhe. Silaa amesema, minara hiyo sita inayojengwa katika wilaya ya Mwanga, itasaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa huduma ya mawasiliano ya simu katika lango hilo na kwa wananchi wa maeneo hayo kwa ujumla.
Minara hiyo inatengwa kupitia mradi wa kimkakati wa ujenzi wa minara 758 unatekelezwa na Serikali kupitia UCSAF kwenye kata 713 nchini. Kupitia mradi huo, Mkoa wa Kilimanjaro ulipata jumla ya minara 30 ambapo hadi kufikia Aprili 9, 2025 jumla ya minara 20 tayari ilikuwa imewaka na inatoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wa wilaya ya Mwanga, jumla ya minara sita inajengwa, ambapo mpaka sasa jumla ya minara 3 tayari imekamilika na inatoa huduma. Ujenzi wa minara mingine 18 iliyosalia unaendelea katika hatua mbalimbali za utekelezaji.