Kilombero
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Wakili Dustan Kyobya amekipongeza Chama cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) kwa kutangaza utalii wa ndani.
Mhe. Kyobya ameyasema hayo leo tarehe 12 Aprili, 2025 mara baada ya maafisa hao wa serikali kutembelea hifadhi ya Taifa ya Udzungwa.
Amesema limekuwa jambo jema kwa maafisa hao wa serikali kufika katika hifadhi hiyo ya Taifa na kujionea vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo kwasababu wanayo nafasi kubwa ya kutangaza vivutio mbalimbali hapa nchini.
“Nimefarijika niliposikia kundi hili kubwa linafika katika wilaya yetu kubwa ya kimkakati kwa sababu ni wilaya inayozalisha umeme, sukari, na mpunga, pamoja na kusimamia uhifadhi.
Hata hivyo amesema wilaya yake inaongoza kwa utalii kupitia hifadhi ya Taifa ya milima ya Udzungwa ambayo imezungukwa vivutio vingi ndani yake.
Mheshimiwa Kyobya amesema Mhe.Rais ameridhia kutoa zaidi ya bililioni 4 kwaajili ya kujenga utalii wa kupita juu ya kamba katika maporomoko ya Sanje yaliyopo milima ya Udzungwa.
Naye, Mwenyekiti wa TAGCO Bw. Karimu Meshack amesema kwamba wametumia Mkutano Mkuu wa Mwaka kuwapatia mafunzo mbalimbali wajumbe hivyo wameona ni fursa pia ya kutembelea hifadhi hiyo kuunga mkono juhudu za Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutangaza vivutio vya utalii na kuhamasisha utalii wa ndani.
Aidha, Meshack ameahidi kutumia Jarida la Serikali Yetu linalomilikiwa na TAGCO kutangaza utalii wa milima na maporoko ya Udzungwa ikiwa ni sehemu ya mchango wa Chama kutangaza utalii wa ndani nchini na nje ya mipaka ya Tanzania.