OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema utekelezaji wa agizo la upandaji wa miti lililotolewa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, ni sehemu kipimo cha utendaji kazi wa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Makatibu Tawala wa Wilaya.
Waziri Mchengerwa amesema hayo, wakati wa hafla ya kutoa tuzo kwa washindi wa shindano la upandaji miti shuleni ilioyofanyika katika shule ya Sekondari Mwambisi Forest iliyopo wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Mhe. Mchengerwa amesistiza kuwa, maelekezo ya Makamu wa Rais ni amri hivyo yatakuwa ni sehemu ya kipimo cha utekelezaji wa majukumu ya Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya pamoja na wasaidizi wao.
“Kaimu Katibu Mkuu peleka maelekezo yangu haya mahususi kwenye sekretarieti zote za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa ili agizo la kupanda miti litekelezwe,” Waziri Mchengerwa amesisitiza.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amewapongeza walimu pamoja na wanafunzi wa shule zote tatu ambazo zimeibuka washindi katika shindano la upandaji miti lililoratibiwa na benki ya NMB.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Benki ya NMB ambaye ni Afisa Mkuu wa Fedha Bw. Juma Kimori, ametangaza washindi katika kampeni hiyo ya upandaji wa miti ambapo Shule ya Sekondari Mwambesi Forest imeibuka mshindi wa kwanza, Shule ya Msingi Ibondo imekuwa ya pili na ya tatu ni Shule ya Sekondari Itimbo.
Benki ya NMB imetoa zawadi ya shilingi milioni 50 kwa mshindi wa kwaza, milioni 30 kwa mshindi wa pili na milioni 20 kwa mshindi wa tatu.