Mkuu wa kitengo cha miamala ya kibenki kutoka NMB, Linda Teggisa akizungumza na waandishi wa habari katika hafla hiyo mkoani Arusha .

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akizungumza katika.hafla hiyo.jijini Arusha



………….
Happy Lazaro, Arusha.
Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali pamoja na mashirika ya kimataifa wameonesha kuvutiwa na vivutio vilivyoko nchini huku wakiahidi kuiongezea nguvu Tanzania katika kutangaza vivutio hivyo katika nchi zao.
Wakizungumza jana kwenye hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa na Benki ya NMB kwa kushirikiana na Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki, mabalozi hao wamesema kuwa Tanzania imebarikiwa kwa kiasi kikubwa katika utunzaji wa bioanuwa hali inayostawisha asili yake ya kimazingira lakini pia wanyama pori.
Mabalozi hao wameyasema hayo jijini Arusha ikiwa ni siku ya tatu ya safari yao ya kutembelea vivutio mbalimbali vilivyoko nchini iliyopewa jina la ‘Diplomatic Safari Tour’.
Balozi wa Kenya Nchini Tanzania, Issack Njega ameishukuru Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki, kwa kuandaa safari hiyo ambayo amesema kuwa itakuwa ya mafanikio makubwa katika kuitangaza vivutio vya Tanzania.
“Tumeona vivutio vingi katika hifadhi ya Serengeti ambayo ndio kubwa kwa Afrika na yenye hadhi na sifa kubwa duniani kwa vivutio vya utalii hadi kupata tuzo nyingi, na sisi tumekubali kweli inastahili kwa upekee iliyonayo” amesema.
Ametumia nafasi hiyo kuomba serikali ya Tanzania kuimarisha mashirikiano zaidi na Kenya katika kutangaza vivutio vyao hasa vile vinavyovuka mipaka kama hifadhi hiyo ya Serengeti ambayo inapakana na hifadhi ya Masai Mara ya Kenya ambayo misafara mikubwa ya nyumbu huhama kwa kupokezana.
Balozi wa Burundi nchini Tanzania Leontine Nzeyimana amesema kuwa Mafanikio ya Tanzani katika utunzaji wa bioanuai imekuwa rafiki kwa wanyama na kuleta uasili wake hivyo kuahidi kutangaza vivutio hivyo kwa wananchi wa Burundi kuja kutembelea Tanzania.
“Kwanza mimi sijawahi kufika katika hiyo mbuga ya Serengeti wala Ngorongoro na kubwa zaidi nilikuwa naogopa kupanda hiyo puto (Baloon) lakini nilipohamasishwa na kupanda hakika nimefurahi na nitarudi tena na tena na kuwaleta wenzangu wengi”.
Amesema kuwa Raia wengi wa Burundi wamekuwa wakitumia gharama kubwa kwenda nchi za Ulaya kipindi cha likizo au mapumziko yoyote ya kujipongeza kwa ajili ya kutafuta upekee hivyo sasa itakuwa wakati mzuri kwake kuwajulisha kuwa upekee huo upo zaidi Tanzania.
“Pale Ngorongoro nimeona watanzania walivyobarikiwa hasa baada ya kubahatika kuona wanyama wengi kwa wakati mmoja wakiwemo wale wakubwa watano (Big five) hivyo nikirudi Burundi nitaawaambia wenzangu hapa ndio sehemu sahihi na sio hata ghali maana watatozwa bei ya mwanajumuya wa Afrika mashariki” .
Balozi wa Comoro, Dr Ahamada El Badaoui Mohamed amesema kuwa imekuwa wakati mzuri kwake kutembelea hifadhi ya Serengeti na Ngorongoro na kuona wanyama na vivutio vingine.
Amesema mazingira asilia yamemfurahisha zaidi kwani ni rafiki na inaweza kuwa tiba hata kwa wanadamu wanaopitia msongo wa mawazo.
“Mimi nimetembea nchi nyingi sana na wanyama wako kila mahali lakini Tanzania ina upekee wa asili kuanzia bioanuai za wanyama, wadudu na mimea na zaidi nimevutiwa na mazingira asilia” amesema na kuongeza;
“Naishauri Tanzania kuhakikisha wanaongeza nguvu ya kutangaza vivutio hivi na mkifanikiwa mnaweza kuwa nchi iliyoendelea kwa kuingiza mapato mengi kwenye utalii pekee, uzuri mimi naenda kuanza kuwatangaza na naahidi wengi watakuja”.
Nae Mkuu wa kitengo cha miamala ya kibenki kutoka NMB, Linda Teggisa amesema kuwa lengo la kuwakutanisha wadau hao wakiwemo Mabalozi na Wakuu wa Misheni za Kidiplomasia, pamoja na wawakilishi wa taasisi za kimataifa ni kuwajulisha masuluhisho ya kifedha wanayotoa hasa za kidigitali na katika sekta ya utalii.
“Masuluhisho yapo mengi ambayo tumewaambia yenye mlengo wa kujenga uwezo wao wa kirasilimali hasa mitaji na mikopo kununua vifaa vya kazi kama magari, na vifaa vinginevyo”.
Amesema kwasasa wanawekeza nguvu kubwa katika kutoa huduma za kidigitali ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
“Tunafanya hivi kwa sababu kwa sasa tunaona zaidi ya asilimia 94 ya miamala yetu inafanywa kidigitali hivyo nguvu yetu pia tunawekeza zaidi huko kuhakikisha hakuna mteja anakwamba kupata suluhisho la kifedha popote anapokuwa nchini na nchi za nje”amesema Linda.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa amesema kuwa wizara yake imeandaa safari hiyo ili kuwapa fursa ya wataalamu hao wa kidiplomasia kuona vivutio vilivyoko nchini kama sehemu ya kukuza mahusiano .
“Lakini pia tunalenga kukuza utalii ambao unaelekea kuwa uti wa mgongo wa Taifa letu, kwani kwa sasa unachangia asilimia 25 ya pato la taifa na tunataka ifikie angalau nusu ya makusanyo nchini kwa kuwa na watalii hata zaidi ya milioni saba kwa mwaka”.
Amesema kuwa ziara hiyo ya awamu ya kwanza imekuwa na wajumbe 25 kutoka nchi mbalimbali na lengo ni kutembeza wajumbe wote 93 walioko na wanaofanya kazi na Tanzania.
“Wajumbe hawa wametembelea Mbuga ya Serengeti, Ngorongoro na wataenda Zanzibar kujionea vivutio vilivyoko kule pia na tunaamini watakuwa mabalozi wazuri wan chi yetu” amesema Balozi Said Shaib Mussa